Patanisho: Jamaa atemwa na mkewe mjamzito kwa kuchelewesha mahari

Muhtasari

•Kiplagat alieleza kwamba mkewe  aliondoka nyumbani bila kumuarifu na kumuacha na wasiwasi mwingi kwani hakuelewa kilichomshinikiza aende.

•Kiplagat aliweka wazi kwamba bado hajamlipia mkewe mahari licha ya kuwa hapo awali wakwe wake tayari walikuwa wameanza kuidai.

•Shangazi ya Chebet alipopigiwa simu alisikika mwenye hasira tele na akuagiza Kiplagat amnunulie mkewe simu ili waweze kuwasiliana moja kwa moja.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Hosea Kiplagat (27) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe  Caroline Chebet (25) ambaye alimuacha miezi miwili iliyopita.

Kiplagat alieleza kwamba mkewe  aliondoka nyumbani bila kumuarifu na kumuacha na wasiwasi mwingi kwani hakuelewa kilichomshinikiza aende.

Wawili hao wamekuwa kwa ndoa kwa kipindi cha mwaka mmoja na wanatarajia mtoto pamoja hivi karibuni kwani Chebet aliondoka akiwa mjamzito.

"Nilikuwa Kikuyu, aliondoka bila kuniambia ametoka. Nilipompigia simu alikataa kushika na akaiwacha nyumbani akaenda hivo tu. Tulikosana kitambo sio hivi karibuni. Ilikuwa kukosana kidogo kama kumpiga kofi hivi tukakosana kidogo tu akatoka. Nilimchapa kwa sababu ya hasira tu kidogo. Hiyo iliisha na tukakaa tu vizuri" Kiplagat alieleza.

Alieleza kwamba wiki mbili  zilizopita alikuwa amefanya juhudi za kuwasiliana na mkewe ila shangazi yake akawazuia kuzungumza zaidi.

Hata hivyo Kiplagat aliweka wazi kwamba bado hajamlipia mkewe mahari licha ya kuwa hapo awali wakwe wake tayari walikuwa wameanza kuidai.

"Bado sijajipanga vizuri na siwezi enda kuiba kwa sababu ya kutaka kuoa. Lazima niende nitafute ndio niwapatie. Anataka tu niende huko aninyanyase kwa sababu pale ni pesa wanahitaji. Chebet aliniambia eti anahitaji tuende tuketi aite watu wajomba wake tuzungumze" Kiplagat alisema.

Kwa kuwa Chebet hakuwa na  simu, Kiplagat alipatiana namba ya shangazi ambaye wanaishi pamoja naye ili waweze kuwasiliana. 

Hata hivyo shangazi ya Chebet alipopigiwa simu alisikika mwenye hasira tele na akuagiza Kiplagat amnunulie mkewe simu ili waweze kuwasiliana moja kwa moja.

"Mwambie anunulie bibi yake simu na simu yangu asifanye utoto. Mwambie sitaki ujinga. Hii simu ni yangu si ya bibi yake. Apeleke maneno kanisani" Shangazi ya Chebet alisema.

Kwa kuwa hakupata nafasi ya kuzungumza na mkewe, Kiplagat alimsihi Chebet hewani arudi ili waweze kujenga familia pamoja. Alimhakikishia kwamba anampenda sana.