Patanisho: Jamaa atemwa kwa kupigia baby daddy wa mkewe simu na kumtumia picha yao pamoja WhatsApp

Muhtasari

• Mbegu alipigia baba ya mtoto wa Sandra na kumfahamisha kuwa yeye ndiye alikuwa amemyakua mpenzi wake wa zamani kisha akamtumia picha ambayo walikuwa wamepigwa pamoja ili aamini.

Ghost studioni
Ghost studioni
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Joshua Mbegu (26) kutoka Kayole alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Melika Sandra (26)  ambaye walikosana naye mwezi wa nane mwakani.

Mbegu alidai mkewe aliondoka kwa kuwa alishuku kwamba jamaa huyo alikuwa hampendi mtoto ambaye alikua naye kwa ndoa.

Alisema kwamba Sandra alipoondoka alimfungia njia zote ambazo angeweza kuwasiliana naye na kutokana na hayo juhudi zake zote za kumfikia hazijafua dafu.

"Tatizo ni kuwa alikuja na moto. Wakati tulikuwa tunawasiliana kwa nyumba aliona ni kama nachukia mtoto wake. Ilikuwa ni ile tu najarIbu kurekebisha mtoto akikosa. Mtoto ana miaka mitatuAlitoka mwezi wa nane nimejaribu kumtafuta imekuwa ngumu. Aliniweka blacklist. Nikijaribu kumpigia na simu nyingine punde tu anaposikia sauti yangu anakata" Mbegu alisema.

Mbegu alidai mke wake alikasirika zaidi na kuondoka baada yake kupigia mama mkwe simu na kumwambie aende achukue mtoto.

"Mama mkwe aliniambia kama mimi ndiye naishi na binti yake ni sawa. Ilifika mahali nikaita mamake kisiri akaja kwangu akachukua mtoto akaenda naye nyumbani. Alisema kwamba simtaki akakasirika akaenda" Alisema.

Juhudi za Ghost kufikia Bi. Sandra ziliangulia patupu ila mama mkwe alikubali kuzungumza na kufichua mengi zaidi kuhusu mzozo kati ya jamaa huyo na binti yake.

Mama mkwe alifichua kwamba Mbegu alipigia baba ya mtoto wa Sandra na kumfahamisha kuwa yeye ndiye alikuwa amemyakua mpenzi wake wa zamani.

Alisema bintiye alikuwa anatazamia kurudiana na kufunga ndoa na baba ya mtoto wake ila hali ilibadilika baada ya Mbegu kumpigia simu.

"Sandra ana mtoto. Josh alipigia baba ya mtoto simu akamwambia yeye ndiye ako na Sandra. Baba ya mtoto alitaka warudiane na Sandra ili walee mtoto pamoja. Ilipofikia pale baba ya mtoto akakasirika akakataa Sandra. Sandra alisema kwa kuwa Joshua alikuwa amemharibia maneno basi hamtaki tena." Alisema Mama Sandra.

Ulikosea sana kupigia baba mtoto wa Sandra simu. Hungempigia Brian simu, Hiyo ndiyo ilimkasirisha sana.Hata ulitumia Brian picha mkiwa na Sandra WhatsApp" Mama Sandra aliambia Mbegu.

Mama mkwe alimfichulia Joshua kwamba Sandra alikuwa amefanya maamuzi ya kusonga mbele na maisha yake na hakumtaka tena maishani.