Patanisho: Jamaa aachwa kwa 'kuiba' pesa za matanga

Muhtasari

•Karimi alisema ndoa yake ya miaka miwili ilisambaratika wakati mke wake alipoteza pesa za matanga na kudai kuwa ni yeye aliziiba. 

•Karimi alidai mkewe alichukua hatua isiyo na mantiki alipogura ndoa baada ya kumsingizia kuchukua pesa zile.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Joseph Karimi Ndungu (32) kutoka Nakuru alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Leah Njunge (32) ambaye walikosana mwezi Septemba kufuatia mzozo wa pesa.

Karimi alisema ndoa yake ya miaka miwili ilisambaratika wakati mke wake alipoteza pesa za matanga na kudai kuwa ni yeye aliziiba. 

Aliapa kuwa hakuchukua pesa zile alizodai kuwa elfu tatu huku akisema mkewe hata hakuwa amemfahamisha kuzihusu.

"Ilikuwa ile pesa ambayo ikichangwa kwa matanga familia hugawia kila mtu. Alipokuja nyumbani baada ya kugawiwa hata hakunijulisha kuhusu pesa yoyote. Asubuhi na mapema alianza kuniambia eti alipoteza pesa. Nilimuuliza ni pesa gani akaanza kupora mfuko akaniambia eti ni mimi nimezichukua. Nilimwambia labda aliweka mahali kisha akasahau. Mimi mbele ya Mungu na Wakenya wote hakuna pesa yoyote nilichukua ama kuona mahali. Aliniambia ilikuwa elfu tatu na mia tatu" Karimi alisema.

Karimi alidai mkewe alichukua hatua isiyo na mantiki alipogura ndoa baada ya kumsingizia kuchukua pesa zile.

"Nilimwambia alikuwa ananitafuta tu kwani hakuna pesa nilichukua. Sijawahi kula jasho ya mtu. Mimi ni hasla anayetafuta pesa zake kila siku. Aliingia kwa nyumba usiku. Mimi nilikuwa nimeingia saa mbili usiku. Tulilala alafu kesho yake nikaamka nikaenda kazi zangu za kawaida.Kurudi akaniambia kunapesa  alipoteza. Nilimwambia atafute polepole kwani huenda alikuwa amesahau ama akaacha kwa matanga badala ya kunisingizia eti nimezichukua" Alisema Karimi.

Alisema hatua zote ambazo alikuwa amepiga kujaribu kuelewana na mke wake hazikuwa zimefua  dafu.

Leah alipopigiwa simu alisita kuzungumza tena punde baada ya kufahamishwa kuwa mumewe alitaka kumuomba msamaha.

Karimi alikubali hali ilivyokuwa ila akamsihi Leah akubali kumsamehe iwapo kuna makosa yoyote ambayo alikuwa amemtendea