Patanisho: Jamaa atemwa na mke wake mjamzito kwa sababu ya ulevi

Muhtasari

•Shaulin alisema mke wake wa miaka miwili alimuacha mnamo mwezi Novemba baada yake kurudi nyumbani akiwa amebugia vikombe kadhaa vya mvinyo.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha Shauline Kunani (28) kutoka Malaba alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Rossy Angatia (26).

Shaulin alisema mke wake wa miaka miwili alimuacha mnamo mwezi Novemba baada yake kurudi nyumbani akiwa amebugia vikombe kadhaa vya mvinyo.

Alisema wakati alifika nyumbani mkewe alianza kumkorofisha na hata kumsukuma chini akaanguka kabla ya kuagiza bodaboda na kuenda.

"Tulianza uhusiano akiwa na mtoto wa miaka miwili, hivi sasa  ana ujauzito wangu. Siku moja nilitoka kwa nyumba mwendo wa saa nne nikaenda kutembea na nikakunywa kidogo. Kurudi kwa  nyumba hivi nikapata amekasirika akaanza vita. Alinisukuma nikaanguka kwa sababu nilikuwa nimelewa kidogo kisha akapigia mtu wa pikipiki simu, akachukua mfuko na akaenda hivo tu. Hata sikuwa nakunywa kila siku!" Shaulin alisimulia.

Alisema juhudi zake za kujaribu kumshawishi mkewe arudi nyumbani zimekuwa zikigonga mwamba kwani amekuwa akidai kwamba angali anafikiria.

"Nimengoja sana sioni akirudi ndio maana nimeileta Patanisho. Sijawahi kumpiga, hiyo siku pekee ndio nilijaribu kumpiga kofi mbili. Sikuwa na mipango ya kando, ilikuwa pombe tu" Alisema.

Rossy alipopigiwa simu ilionekana kama kwamba hakuwa tayari kuzungumza na mumewe kwani Gidi alipowapatia nafasi ya kuzungumza na kuelewana alikata simu yake mara moja.

Shaulin alisikika kutopendezwa na jambo hilo na hata kumpa vitisho mkewe baada ya kugundua kuna uwezekano mkubwa wa kutomrudia.