Patanisho: Mwanadada agura ndoa baada ya kushambuliwa na mazingaombwe usiku

Muhtasari

•Winnie alisema alijaribu kumueleza mumewe kuhusu mateso ambayo alikuwa anatendewa na majini usiku alipokuwa amelala ikiwemo kunyongwa na kubebwa hadi baharini  ila hakumuamini. 

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho mwanadada aliyejitambulisha kama Winnie Mutuku (26) kutoka Machakos alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mumewe Francis  Mutui (32) ambaye walikuwa naye kwenye ndoa  kwa miaka mitatu hadi walipotengana takriban miezi miwili iliyopita.

Winnie alisema alifanya maamuzi ya kugura ndoa yake mnamo mwezi Novemba mwaka jana baada ya kugundua nyumba ambayo walikuwa wanaishi ilikuwa imekabiliwa na mazingaombwe.

Alisema alijaribu kumueleza mumewe kuhusu mateso ambayo alikuwa anatendewa na majini usiku alipokuwa amelala ikiwemo kunyongwa na kubebwa hadi baharini  ila hakumuamini. 

"Nilikuwa nalala naona watu wawili wazee, mama na baba. Mara nyingi walikuwa wananinyonga, mara wananibeba usiku  wananipeleka baharini. Nilipojaribu kumueleza hakuwa ananielewa. Nilipoona imekidhiri  niliamua kutoka na kurudi kwetu.  Tulikuwa tunaishi Mombasa sehemu za Kongowea" Winnie alisimulia.

Alikiri kwamba alichukua simu ya mumewe na kujitumia shilingi elfu tisa kwa kuwa hakuwa na nauli kisha akaondoka na kurudi kwao Machakos.

Mwanadada huyo alisema alifanya maamuzi ya kuondoka baada ya kunyongwa usiku kucha na watu asiyowafahamu kisha siku iliyofuata akatembelewa na mmoja wao.

"Sikuwa na nauli, nilichukua simu yake nikatoa pesa  na  nikaamua kurudi nyumbani kwa sababu hakuwa ananielewa. Mara ya mwisho ndio niamue kutoka nirudi nyumbani nilinyongwa  hadi nikapoteza sauti ikaisha kabisa. Siku iliyofuata  mwenye nilikuwa naona kwa ndoto akakuja hadi nyumbani. Alichoniambia kilinishtua sana. Alinipata kwa nyumba akaniambia eti nimewasumbua sana. Niliona heri nirudi kwetu" Alisema.

Winnie alisema kwamba mumewe hakuwa anatembelewa na watu hao ambao walikuwa wanamshambuliwa usiku.

Alifichua kwamba mumewe alighadhabishwa sana na kitendo chake cha kutoa pesa kwa simu yake bila idhini.

Bw Francis alipopigiwa simu hakutaka kuzungumza kwani alidai alikuwa safarini akielekea kazini.

Winnie alifichua kwamba mumewe bado anaishi kwa nyumba ile licha ya yote ambayo yeye mwenyewe alikuwa anapitia pale.

Alisema angependa kumrudia mumewe ila kwa masharti kwamba lazima ahame kutoka kwa nyumba ile.