Patanisho: Jamaa avurugana na shemejiye baada ya kuvamia shamba lake na kuvuna mahindi yake yote

Muhtasari

•Geoffrey alisema Bi.  Jane alishirikiana na watoto wake kushambulia shamba yake na kuvuna mahindi yote baada yake kukosana na mkewe. 

•Jane alimshauri Geoffry aandae kikao na mashemeji wake wengine ili wasuluhishe mzozo uliopo huku akimweleza kwamba matendo yake yalimshtua sana baba mkwe na hata kuathiri afya yake vibaya.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho jamaa aliyejitambulisha kama Geoffrey (30) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na shemeji yake Jane (40) ambaye walikosana kufuatia mgogoro uliohusisha mahindi.

Geoffrey alisema walikosana na Jane mnamo Julai 2020 baada ya kumshtaki kwa polisi kwa polisi kwa kuvuna mahindi yake.

Alisema Bi  Jane alishirikiana na watoto wake kushambulia shamba lake na kuvuna mahindi yote baada yake kukosana na mkewe. Hata hivyo alikiri kwamba kwa sasa anajuta hatua aliyopiga kwa sababu shemeji huyo wake alimsaidia sana kila alipokabiliwa na shida.

"Wakati nilikosana na mke wangu, nilirudi kazini. Baada ya kurudi shemeji yangu aliingia kwa shamba yangu na watoto wake na kuvuna mahindi. Niliambia ndugu zangu wakaenda huko na kumshtaki" Geofrrey alisema.

Bi Jane alipopigiwa simu alisema kwamba yuko tayari kumsamehe Geoffrey iwapo tayari amejuta makosa yake.

Hata hivyo alimshauri aandae kikao na mashemeji wake wengine ili wasuluhishe mzozo uliopo huku akimweleza kwamba matendo yake yalimshtua sana baba mkwe na hata kuathiri afya yake vibaya.

"Alisababisha baba yangu mzazi kuwa mgonjwa zaidi. Hiyo kitu ilimshtua sana ata saa hii bado ni mgonjwa. Ningependa kumpa nafasi aende aongee na wazazi, makosa hutokea. Wasuluhishe waendelee kuishi pamoja. Kwa upande wangu sina shida" Jane alisema.

Jane alimkosoa Geoffrey kwa kushambulia mashemeji wake baada ya kutofautiana na mkewe badala ya kuandaa kikao nao ili kujaribu kutafuta suluhu.

Geoffrey alikubali ushauri wa bi Jane na kuahidi kwamba angefunga safari ya kwenda kwa wakwe wake ili kusuluhisha mzozo kati yao.