Patanisho: Jamaa avurugana na mkewe baada ya kurudi nyumbani bila pesa za chakula

Muhtasari

•Jacob alisema mvurugano kati yake na Ruth ulitimbuka baada yake kurejea nyumbani kutoka kazini bila pesa hata ya kununua chakula.

•Alisema walivurugana na mkewe kwa muda kabla ya kupanga virago vyake na kuondoka pale nyumbani.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost kitengo cha Patanisho jamaa aliyejitambulisha kama Jacob alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Ruth ambaye alidai walitengana baada ya kutofautiana nyumbani.

Jacob alisema mvurugano kati yake na Ruth ulitimbuka baada yake kurejea nyumbani kutoka kazini bila pesa hata ya kununua chakula.

Alidai hawakulipwa chochote mahali ambapo alikuwa ameenda kufanya kazi ya ukulima na badala yake waliambiwa wasubiri malipo baadae. Alieleza kwamba mkewe alikosa kuelewa hali ilivyokuwa licha yake kujaribu kumweleza.

"Nilitoka nikaenda kazi ya ukulima. Nilienda nikalima ila nilipomaliza sikulipwa. Nilirejea nyumbani nikaambia mke wangu kwamba sijalipwa na nimeambiwa nisubiri pesa hadi jioni. Alianza kusema kwamba huwa naenda kwa wanawake wengine. Nilikana na kusisitiza kwamba sikuwa nimelipwa.

Alikasirika tukaanza kugombana. Aliniuliza kama naona maisha yangu pamoja na yeye kisha akasema kwamba hatungeweza kuendelea. Mimi nilimwambia hakuna shida na nitapanga vitu vyangu niende kazi" Jacob alisema.

Jacob alisema walivurugana na mkewe kwa muda kabla ya kupanga virago vyake na kuondoka pale nyumbani.

Alisema baadae mkewe alimpigia simu mara kadhaa akimuomba hela na mara nyingine akimgombanisha.

"Aliniambia nimtumie pesa nikamdanganya kwamba ningemtumia Sh3,000. Baada ya hapo akanizimia simu... Ningependa turudiane kwa sababu tulikotoka ni mbali" Alisema.

Jacob aliweka wazi kwamba wakati walipokuwa katika mahusiano walisaidiana katika mambo mbalimbali ya kinyumbani yaliyohitaji fedha.

Juhudi za kumpata Bi Ruth kwa simu ziliangulia patupu licha ya Gidi kujaribu kumpigia mara kadhaa.

Je una ushauri gani kwa Jacob?