Patanisho: Mwanadada alalamika kuhangaishwa na majini waliotumwa na wanafamilia wa mumewe

Muhtasari

•Opiyo alifichua kuwa baada ya mama yake kuaga mkewe alianza kudai anarogwa na mama zake wawili wa kambo na akaanza kutafuta usaidizi wa maombi.

•Grace alisema kuwa alibadilisha kanisa katika juhudi za kutafuta suluhu ya masaibu ambayo alikuwa anapitia kwa boma.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Benjamin Opiyo alituma ujumbe akiomba kusaidiwa kuelewana na mke wake Grace Atieno kutokana na ukosefu wa utulivu kwa boma yao.

Opiyo alisema hali ya wasiwasi ilianza kusheheni jkatika ndoa yao punde baada ya mama yake kufariki mnamo mwezi Juni mwaka jana.

Alieleza kuwa baada ya mama yake kuaga, mkewe alianza kudai anarogwa na mama zake wawili wa kambo na akaanza kutafuta usaidizi wa maombi. Opiyo alisema hatua hiyo ya mkewe ilimsababishia hasara kubwa ya kifedha.

"Mama aliaga mwezi Juni mwaka jana. Hapa nyumbani tunaishi na wanawake wengine wawili kwa kuwa babangu alikuwa na wanawake watatu. Mama yangu alikuwa mke wa kwanza, sasa tumebaki na wengine wawili. Bibi yangu alianza kusema hao wanawake wawili wanamroga. Tuko na duka kubwa na yeye hafanyi kazi. Kila anapoona wamama hao anaanza kushtuka. Amenishtua moyo kabisa, nataka nimtoe huku aende kwao atulie kwanza. Mamake na ndugu zake wakimshauri atarudi" Opiyo alisimulia.

Jamaa huyo alieleza kuwa mkewe amekuwa akipiga hatua za kutatatisha ikiwemo kubadilisha kanisa katika juhudi za kutafuta suluhu ya tatizo lake.

Grace alipopigiwa simu alisisitiza kwamba kunao wanafamilia wa mumewe ambao walikuwa wanamtumia mazingaombwe wakikusudia kuwafurusha kutoka kwa shamba lao.

"Hizi ni majini ambazo hao watu wametuma ili atoke kwa boma. Wanasema atoe hati ya umiliki wa shamba na hana. Wanang'ang'ania shamba. Wanatafuta njia zote wanisukume niende, sio yeye anataka niende. Wanasukuma majini ili nitoroke wabaki na shamba yeye abaki akihangaika" Grace alisema.

Grace alisema kuwa alibadilisha kanisa katika juhudi za kutafuta suluhu ya masaibu ambayo alikuwa anapitia kwa boma.

Hata hivyo alisema ako tayari kurekebisha mienendo ila akamwomba mumewe amruhusu aende kwa kanisa la chaguo lake na aombe kwa amani.