Patanisho: "Hayo mapenzi yako ya kijinga sitaki, sio mapenzi original!" Mwanadada amkemea mumewe

Muhtasari

•Ishmael alieleza kuwa ndoa yake ya miaka sita ilisambaratika mwaka mmoja uliopita kufuatia mzozo wa kinyumbani.

•Alicia alifichua kuwa Ishmael hakuwahi jitambulisha kwao nyumbani katika kipindi cha miaka sita ambacho walikuwa pamoja.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, Ishmael  (27)  alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mkewe Alicia Bevaline. (23)

Ishmael ambaye mwanzoni alidanganya jina lake halisi alieleza kuwa ndoa yake ya miaka sita ilisambaratika mwaka mmoja uliopita kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Ishmael alisema alipata ajali kidogo na alipofika nyumbani wakavurugana na mkewe kuhusiana na masuala ya kinyumbani nusura amchape. 

"Aliniuliza naenda wapi ilhali nilikuwa mgonjwa. Mimi sikumjibu kwa sababu kuna mtu ambaye alikuwa na pesa yangu aliniambia tupatane mahali anipatie. Kurudi tukaanza kuzozana kuhusu mambo ya nyumba. Niliona ili nisimchape kutokana na hasira  ni heri niende nikae kwa mamangu kidogo. Kurudi kwa nyumba nilipata akiwa ametoka akaenda," Ishmael alisimulia.

Ishmael alisema amekuwa akijaribu kushawishi mkewe arudi ila juhudi zake zote zimekuwa zikigonga mwamba.

Alicia alipopigiwa simu alifichua kuwa kulitokea migogoro mingi kwenye ndoa yake  na Ishmael. Alifichua kuwa Ishmael hakuwahi jitambulisha kwao nyumbani katika kipindi cha miaka sita ambacho walikuwa pamoja.

Mwanadada huyo pia alimshtumu Ishmael kwa kukosa ukomavu.

"Hayo mapenzi yako ya kijinga nilikwambia sitaki. Nilishakukataza. Kwani nitashinda tu kwa njia nikienda nikirudi?! Ni mara ngapi tumekosana ukiomba msamaha kisha narudi? Mapenzi yako nilisahau kitambo juu ni ya ujinga, sio mapenzi original. Bado uko na utoto ndani yako, " Alicia alisema

Juhudi zote za Ishmael kujitetea ziliangulia patupu kwani Alicia alisisitiza kuwa hayuko tayari kurudiana naye.