Patanisho "Aliniambia kuwa mtoto sio wangu!" Jamaa alalamika dhidi ya mkewe

Muhtasari

•Isaac alisema kwamba ndoa yake ya miaka mitano ilisambaratika wiki tatu zilizopita baada ya mkewe kukataa agizo lake la kusitisha urafiki na jirani 'mwenye fitina'.

•Linda alisema kwamba kila mumewe anapotofautiana na mtu yeyote huwa anaonya familia nzima kutoshirikiana nao.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Isaac Omondi (27) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe Linda Anyango (22) ambaye walitengana kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Isaac alisema kwamba ndoa yake ya miaka mitano ilisambaratika wiki tatu zilizopita baada ya mkewe kukataa agizo lake la kusitisha urafiki na jirani 'mwenye fitina'.

"Nilikuwa namkataza urafiki na mwanamke huyo anakata. Watu walikuwa wanasema kwamba ako na fitina mingi, eti huwa anakosanisha watu na mabibi zao. Huwa hatoki kwa nyumba. Sikutaka bibi yangu atembee naye kutokana na mambo ambayo nilisikia kumhusu.

Kuna siku nilisikia ati walienda kutembea, sijui walienda wapi.  Nilitoka kazi nikamwambia sitaki atembee na huyo mama. Asubuhi nilipoamka nilimkataza mtoto wangu kucheza na watoto wa jirani huyo. Baada ya hapo mke wangu aliniambia kuwa mtoto ati sio wangu, ati huwa simshughulikii. Saa hii anaishi na msichana mwingine," Omondi alisema.

Linda alipopigiwa simu alifichua kwamba mumewe amekuwa akimpiga mara kwa mara. Alisema kwamba kila mumewe anapotofautiana na mtu yeyote huwa anaonya familia nzima kutoshirikiana nao.

"Huwa anapigana mara kwa mara. Akikosana na mtu huwa anataka usiongee naye. Alikosana na huyo mama na sasa hataki niongee naye ama watoto wake wacheze na wangu," Alisema.

Linda aliomba mumewe ampatie muda wa kufikiria kwanza kabla ya kufanya maamuzi ya kurudi.