"Siwezi kurudi! Nilimpea ruhusa aoe" Mwanadada amtema mumewe baada ya kutofautiana na mama mkwe

Muhtasari

•Christopher alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka kumi mnamo Januari mwaka uliopita baada ya kutofautiana na mama mkwe.

•Violet alipopigiwa simu aliweka wazi kwamba hayupo tayari kurejea katika ndoa yake na Christopher. 

Gidi na Ghost asubuhi
Gidi na Ghost asubuhi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Christopher Imbwaga alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe Violet ambaye walitengana mwaka jana.

Christopher alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka kumi mnamo Januari mwaka uliopita baada ya kutofautiana na mama mkwe.

Alisema kwamba wamekuwa wakiwasiliana na mkewe na tayari amemuahidi kurudi kabla ya mwezi Agosti. Hata hivyo, Christopher alisema angependa Violet amhakikishie kuwa atarudi.

"Mama hakutaka kukaa na mke wangu na watoto.  Baba aliaga 2014, mama hakuwa na kazi. Mama alikuja na watoto wengne ili watawale mali ya babangu. Mke wangu alikasirika akaenda. Tumekuwa tukiongea naye. Anasema kuwa atarudi kabla ya uchaguzi," Christopher alisema.

Violet alipopigiwa simu aliweka wazi kwamba hayupo tayari kurejea katika ndoa yake na Christopher. Alisema kwamba angependa kulea watoto wao wawili pekee yake.

"Siwezi kurudi. Nilimpea ruhusa aoe. Wacha nilee watoto wangu. Yeye na mamake wako na makosa. Sitaki," Violet alisema kwa ukali.

Christopher alikubali maamuzi ya mkewe na kumuomba aweze kutunza watoto wao vizuri. 

"Siku ingine akisikia nimeoa asikuje kulalamika. Nimekubali. Watoto wangu aweze kuwachunga vizuri," Christopher alisema.