Patanisho: Jamaa wa bodaboda aachwa kwa kunyemelea rafiki wa mkewe

Muhtasari

•Suzzie alisema aligura ndoa yao ya miaka minne baada ya kumpata mumewe akimtongoza rafiki yake kwa simu.

•Suzzie alisisitiza kuwa anampenda sana mumewe na kumuomba amtumie fedha za kutayarisha mazishi ya marehemu babake

Ghost Mulee na Gidi Ogidi
Ghost Mulee na Gidi Ogidi
Image: RADIO JAMBO

Mwanadada Peris Suzzie alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mumewe Kihiu Njuguna ambaye walikosana naye takriban miezi miwili iliyopita kutokana na mambo ya mpango wa kando.

Suzzie alisema aligura ndoa yao ya miaka minne baada ya kumpata mumewe akimtongoza rafiki yake kwa simu.

"Nilimpata na rafiki yangu. Walikuwa na mahusiano. Nilipata anamtumia meseji za kimapenzi. Nilipomuuliza akakasirika, akawa haniongeleshi. Nilipoona amenikasirikia nikaamua kuondoka," Suzzie alisimulia.

Mwanadada huyo alisema anamnyooshea mumewe kidole cha lawama kwa yaliyotokea kwani yeye ndiye alikuwa anamtaka rafikiye.

Suzzie hata hivyo alisema mumewe alimhakikishia kuwa amekoma tabia hiyo.

"Aliniambia ati waliachana na rafiki yangu lakini sina uhakika. Bado tunaongea na rafiki yangu.  Rafiki yangu anasema ata hataki mambo yake eti yeye ndio anamnyemelea," Alisema.

Njuguna hata hivyo alitupilia mbali madai ya mkewe kuwa alikuwa anamtongoza rafiki yake. Alisisitiza kuwa Suzzie pekee ndiye mpenziwe na hana mwingine.

"Hakuna kitu kibaya. Mimi sio shida. Hatujakosana. Sina mwanadada mwingine. Sijanyemelea mwingine," Alisema.

Suzzie alisisitiza kuwa anampenda sana mumewe na kumuomba amtumie fedha za kutayarisha mazishi ya marehemu babake ambaye atazikwa Jumamosi.

Nitumie kakitu tununue kitambaa ya kufunika babangu. Nakupenda kama uji. Ata wewe unajua," Suzzie alisema.

Wawili hao waliweza kupatana huku Njuguna akiahidi kumtafuta Suzzie na kujadiliana zaidi kuhusu suala la kurudiana.