Patanisho: "Sitaki usumbufu wowote!" Jamaa akataa katakata kurudiana na mkewe

Muhtasari

•Mwanadada huyo alisema mumewe alimshtumu kwa kukosa heshima ndiposa wakaafikiana kutengana.

•Josiah alipopigiwa simu alisema kuwa mkewe alimkosea na akakataa katakata suala lao kurudiana.

Ghost Mulee na Gidi Ogidi
Ghost Mulee na Gidi Ogidi
Image: RADIO JAMBO

Jeniffer kutoka Machakos alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mumewe Josiah Otieno ambaye alitengana naye mwezi Februari kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Mwanadada huyo alisema mumewe alimshtumu kwa kukosa heshima ndiposa wakaafikiana kutengana.

"Alikuwa anasema eti huwa simheshimu. Alikuwa anaitisha mtoto tukaamua tuachane. Alipoitisha mtoto nilimwambia haiwezekani kwa kuwa bado ni mdogo. Mtoto alikuwa na mwaka mmoja, miezi sita," Jeniffer alisema.

Alisema baada ya ndoa yake kugonga ukuta alimtuma dadake kwa mumuwe katika juhudi za kujaribu kutatua mzozo wao.

Jeniffer aliweka wazi kuwa mumewe amekuwa akishughulikia mtoto wao ila amekuwa akipinga mazungumzo yoyote naye.

"Kwa sasa ameniblock. Akiskia sauti yangu anakata simu. Huwa anashughulikia mtoto," Jeniffer alisema.

Josiah alipopigiwa simu alisema kuwa mkewe alimkosea na akakataa katakata suala lao kurudiana.

"Hiyo haitawezekana. Nikifanya maamuzi yangu huwa sirudi nyuma. Alinikosea," Alisema Josiah.

Jeniffer alijaribu kumbembeleza mumewe warudiane huku akimhakikishia kuwa bado anampenda ila Josiah akashikilia msimamo wake.

"Sitaki mazungumzo na mtu. Niko na mambo mengi na sihitaji usumbufu wowote. Hii sio mara yangu ya kwanza kusema kuwa nikishafanya maamuzi huwa sirudi nyuma. Hatuwezi kuwa pamoja na huo ndio uamuzi wa mwisho," Alisema Josiah.

Josiah aliendelea kumsihi Jeniffer aendelee kujiangalia vizuri na akatoa hakikisho kuwa ataendelea kushughulikia mtoto wao.