Patanisho: Jamaa atemwa na mkewe mjamzito kwa madai ya kuhanyahanya

Mbugua alisema anashuku mpenziwe tayari yupo kwenye mahusiano mengine licha ya kuwa mjamzito.

Muhtasari

•Mbugua alidai kuwa Bi Wangui aligura ndoa yao ya mwaka mmoja takriban miezi mitatu iliyopita kufuatia mzozo wa kinyumbani.

•Ruth alipopigiwa simu alisita kuzungumzia mzozo wao na kumwelekeza mpenziwe awasiliane naye baadae kwa njia ya simu.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, Chris Mbugua (24) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mpenzi wake Ruth Wangui (22).

Mbugua alidai kuwa Bi Wangui aligura ndoa yao ya mwaka mmoja takriban miezi mitatu iliyopita kufuatia mzozo wa kinyumbani.

"Tulikosana na mke wangu kufuatia mazozano ya nyumbani. Alikuwa anatembea na watu hawafai. Walikuwa wakimdanganya eti nahanya ila sio kweli," Mbugua alisema.

Mbugua alifichua kuwa mpenzi huyo wake alikimbia ndoa yao akiwa na ujauzito wa takriban miezi mitatu.

Alidai kuwa anashuku kuwa mpenzi huyo wake tayari yupo kwenye mahusiano mengine licha ya kuwa na ujauzito wake.

"Nashuku ako na mtu kwa sababu kwa sasa yuko Laikipia na kuna rafiki yangu alinipigia simu akaniambia eti huwa anaonekana na mtu fulani kila wakati. Sijamuona kwa takriban miezi miwili," Alisema.

Mbugua alieleza kuwa angependa kujua ukweli kutoka kwa mpenziwe ili aweze kujua hatua ambayo atachukua.

Ruth alipopigiwa simu alisita kuzungumzia mzozo wao na kumwelekeza mpenziwe awasiliane naye baadae kwa njia ya simu.

"Mimi saa hii siongei. Mimi niko poa. Nipigie simu direct," Ruth alisema.

Gidi alipomueleza  Ruth madai ya mumewe kuhusu kilichowatenganisha na kumtaka aeleze ukweli wake, aliangua kicheko kikubwa kabla ya kukata simu yake.

Mbugua alielekezwa kumpigia simu Ruth ili kujadiliana kuhusu mahusiano yao.

Je, una ushauri upi kwa wawili hao?