Patanisho: "Ukikufa sitakuja matanga yako"- Mwanadada amwambia babake mkubwa

Loreen alisema baada ya kukaa chini na kutafakari alijuta sana.

Muhtasari

•Loreen alifichua kuwa uhusiano wake na babake mkubwa ulisambaratika baada ya kumtumia meseji ya matusi.

•Baba Bruce alisema amekubali ombi la msamaha la mpwa huyo wake ila akamshauri abadilishe tabia zake.

Gidi Ogidi
Image: RADIO JAMBO

 Loreen alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na babake mkubwa Baba Bruce ambaye walikosana naye mwaka jana.

Loreen alifichua kuwa uhusiano wake na babake mkubwa ulisambaratika baada ya kumtumia meseji ya matusi.

Alidai kwamba mzozo kati yao ulitimbuka wakati walipokutana katika matanga iliyofanyika nyumbani kwao kijijini.

"Tulienda matanga kwetu nyumbani na bwanangu. Matanga ilikuwa kwa jirani. Kumaliza tukaenda nyumbani. Baba mkubwa akasema tukae chini kwa nyumba yake. Hakupenda mtindo wa nywele ambao nilikuwa nimenyolewa," alisimulia.

Loreen alisema kwamba baada ya baba yake mkubwa kuchukizwa na mtindo wa nywele yake alimtusi mbele ya kila mtu ambaye alikuwa amejumuika pale wakiwemo bwana yake na wanafamilia wengine.

"Baada ya kurudi kwangu nilimtumia ujumbe wa matusi nikwambia 'Ukikufa sitakuja kwa matanga.. Hakujibu'" alisema.

Alisema baada ya kukaa chini na kutafakari alijuta sana kitendo hicho chake.

Baba Bruce alipopigiwa simu, Loreen alimuomba msamaha kwa matusi ambayo alimminia mwaka jana.

Baba Bruce alisema amekubali ombi la msamaha la mpwa huyo wake ila akamshauri abadilishe tabia zake.

"Nimekusamehe lakini punguza ujinga. Ukitaka kuniambia kitu, jua vile utaniambia lakini ukionja  kitu kidogo kama pombe usiniongeleshe," alimwambia Loreen.

Zaidi ya hayo alimwalika nyumbani kwake kwa sherehe za Krismasi na kuahidi kumchinjia kuku.