Patanisho: Baba amfukuza bintiye kwa panga baada ya kupata ujauzito

Felix alisema mkewe na mama mkwewe walilalamika kuhusu hali ya mfuko wake.

Muhtasari

•Felix alisema mkewe Maureen alitoroka nyumbani na kurudi kwao mwezi uliopita bila kuacha taarifa yoyote wala kutaja sababu.

"Yeye (Felix) ndo alimfanya aache shule. Alimaliza mtihani, nilitaka kumpeleka shule lakini akamdanganya," Mama Maureen alisema.

Ghost Mulee na Gidi Ogidi
Ghost Mulee na Gidi Ogidi
Image: RADIO JAMBO

Kwenye kipindi cha Gidi na Ghost, kitengo cha Patanisho, Felix alituma ujumbe akiomba kusaidiwa kuokoa ndoa yake.

Felix alisema mkewe Maureen alitoroka nyumbani na kurudi kwao mwezi uliopita bila kuacha taarifa yoyote wala kutaja sababu.

Felix alisema mkewe na mama mkwewe walilalamika kuhusu hali ya mfuko wake, sababu anayoshuku ilisababisha yeye kugura.

"Alitoka nyumbani bila kunifahamisha. Nilikuwa nimekuja kazi Nakuru.Nikipiga simu hawashiki," alisema.

Felix alisisitiza kuwa licha ya kutokuwa na uwezo mkubwa wa kifedha alikuwa akimsaidia mkewe na kugharamia mahitaji yake.

"Mimi nilikuwa nikimvumilia. Yeye hangeweza kunivumilia. Nikimpatia pesa anasema ni kidogo. Alikuwa amesema nimnunulie mashine ya blowdry," alisema

"Tulianza uhusiano 2018, tulikuwa tumekaa pamoja kwa mwaka mmoja. Kwao wananijua. Mahari bado sijalipa,"

Felix alisema kwamba alijitosa kwenye ndoa na Maureen baada ya baba yake kumfukuza kwao alipopata ujauzito.

"Baba yao alimfukuza kwao na panga. Baba yao ni mtu analewa. Alimwambia aende kwa mtu alimzalisha," alisema.

Gidi alimpigia simu mamake Maureen ambaye alifichua mengi kuhusu yaliyotokea kati ya bintiye na Felix.

Mama Maureen alidai kwamba Felix alitoka nyumbani na kwenda kazi kwingine bila kumfahamisha mkewe, jambo ambalo liliimjaza hofu moyoni  hadi kumfanya achukue hatua ya kurudi kwao.

"Ukipata kazi lazima unafaa umuambie mke wako. Wewe hukumuambia. Anasema ulioa mtu mwingine. Ulimaliza mwezi mzima huko  na hukumwambia kitu. Alikuja kuniomba sabuni, kumwambia sina akaanza kulia kwa sababu hata wewe hukuwa umempatia pesa. Nilimwambia arudi nyumbani," alisema.

Aliongeza kuwa, "Yeye (Felix) ndo alimfanya aache shule. Alimaliza mtihani, nilitaka kumpeleka shule lakini akamdanganya."

Mama Maureen hata hivyo alimshauri Felix achukue hatua ya kuenda nyumbani ili wapate kusuluhisha mzozo uliopo.