Patanisho: "Aoe ama nimtafutie mrembo!" Mwanadada amwambia mumewe aliyeruka mtoto

Muhtasari

•Ngumbau alisema ndoa yao ya miaka minne ilisambaratika kufuatia mzozo uliochimbuka baada ya kumwekea mkewe hoteli.

•Roselyn alihoji suala la mume huyo wake wa zamani kutoshughulikia mtoto wao tangu kutengana kwao.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, Joseph Ngumbau kutoka Kitui alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mke wake Roselyn ambaye alitengana naye takriban miaka miwili iliyopita.

Ngumbau alisema ndoa yao ya miaka minne ilisambaratika kufuatia mzozo uliochimbuka baada ya kumwekea mkewe hoteli.

"Nilikuwa nimemwekea kazi ya hoteli. Mwanzoni tulikuwa tunafanya naye. Ilifika wakati nikamnunulia simu, ikawa anashinda kwa simu. Niliweka software ilikuwa akiongea inarekodi na hakujua," alisimulia.

"Niliona kuna mtu mwingine alikuwa anaongea nayeye. Nikamwambia aache mambo ya simu. Hapo Akaanza vurugu, nilimrusha akaanguka na nikachukua simu. Alienda kwa nyumba akachukua vitu akaenda kwao,"

Aliongeza, "Nilifuatilia nikajua anaongea na mwanaume mwingine. Walikuwa wanaongea mambo ya urafiki. Sikuelewa alikuwa nani lakini hakuwa mteja wa chakula."

Ngumbau alisema hapo awali alikuwa akiongea na mama huyo wa mtoto wao mmoja na kufichua kuwa alimhakikishia kuwa anaweza kumsamehe lakini hakuna uwezekano wa kurudiana.

Roselyn alipopigiwa simu, Ngumbau alichukua fursa kumuomba msamaha.

Mwanadada huyo hata hivyo aliweka wazi kwamba hayupo tayari kwa wao kurudiana.

"Nilikwambia naweza kukusamehea lakini kurudiana never! Mbona hungenipigia simu ukaenda kwa radio. Tukipendana mbona hukuweka huko? Mbona hukusema tumependa?" Roselyn alimwambia mzazi huyo mwenzake.

Roselyn pia alihoji suala la mume huyo wake wa zamani kutoshughulikia mtoto wao tangu kutengana kwao.

"Huu ni mwaka wa tatu. Unajua chenye mtoto huwa anakula? Unajua chenye huwa anavaa. Hakuwa anasaidia mtoto," alisema.

Alifichua kwamba alimbock Ngumbau baada ya kuwa akimwandikia jumbe za matusi kwenye sehemu ya maoni ya machapisho ya Facebook.

"Atafute mwanamke mwingine aoe. Mimi sina shida ya wanaume. Sitaki mwanaume tena," alisema.

Aidha, alifichua kwamba Ngumbau alikuwa amekana mtoto wao na kuagiza vipimo vya DNA.

"Alikana mtoto akasema sio damu yake. Alisema mtoto hafanani na Yeye. Nilimwambia tuende DNA akakataa. Baada ya kuachana ndio alisema tuende DNA. Sasa nimefungua kitabu mpya, cha kitambo nimefunga," alisema.

Ngumbau hata hivyo alidai kwamba Roselyn ndiye aliyekataa yeye kuhusika katika maisha ya mtoto wao.

"Mwambie aoe ama nimtafutie mrembo. Mimi sina shida. Hata alikuwa ameoa juzi, mimi sikuleta shida," alisema.

Ngumbau alifutilia mbali madai kwamba alikuwa ameoa mwanamke mwingine.

"Mapenzi kwake yashaisha. Nishafanyia mtoto kila kitu, sitaki usaidizi wake kabisa," Roselyn alisema.

Ngumbau hata hivyo alisisitiza kwamba ataendelea kumtafuta mke huyo wake wa zamani hadi warudiane.