Patanisho: "Ako kwa ndoa nyingine lakini anasema sio permanent" Jamaa amsihi ex aliyeolewa arudi

Kerumbo alimtaka mume huyo wake wa zamani asiulize maswali mengi wakati atakaporudi.

Muhtasari

•Julius alisema mke wake aligura ndoa yao ya miaka 17 takriban miaka sita iliyopita na hakumweleza sababu ya kuchukua hatua hiyo.

•Kerumbo alidai kwamba alimtema Bw Julius kwa sababu alikuwa akienda nje ya ndoa sana.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Julius Owanga ,40,  alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mke wake Leonita Kerumbo ,30, ambaye alitengana naye miaka minne iliyopita.

Julius alisema mke wake aligura ndoa yao ya miaka 17 takriban miaka sita iliyopita na hakumweleza sababu ya kuchukua hatua hiyo.

"Tulikuwa tunaishi nyumbani. Tukakuja Nairobi. Mwaka wa 2017, aliamka akaenda na watoto nyumbani. Nilikuwa kazini nikapigiwa simu kuwa bibi yangu ameenda na watoto nyumbani. Sikuwa nimemkosea," alisema.

Alisema kwamba baadaye Bi Kerumbo alirudi jijini Nairobi na kuishi katika mtaa wa Utawala

"Baadaye nilimfuatilia akaniambia atarudi lakini hajawahi kurudi. Ananiambia anakuja lakini hakuji," alisema.

Julius alifichua kwamba mzazi huyo mwenzake kwa sasa anaishi na mwanaume mwingine ila amekuwa akiahidi kurudi.

"Watoto wanateseka. Watoto wako kwetu. Nataka akuje tushughulikie watoto. Anaishi na mwanaume lakini anasema hayuko permanent. Ata watoto wakimpigia simu huwa anasema atarudi," alisema.

Kerumbo alipopigiwa simu alikiri kwamba kwa kweli yuko kwenye ndoa nyingine baada ya kumtema Julius. 

Kerumbo hata hivyo alisisitiza kwamba anapanga kugura ndoa yake ya sasa na kurudi kwa ndoa yake ya kwanza.

"Nitarudi tu. Nitarudi mwezi wa nne. Niko Tassia. Ni ukweli naishi kwa mwanaume mwingine. Nitaachana na huyu mwanaume. Nitarudi niwe na watoto wangu, siwezi kuacha watoto wangu," alisema.

Alipoulizwa jinsi atakavyotoka kwa ndoa yake ya sasa, alisema, "Nitamwambia nataka kurudi kwa ndoa yangu ya kwanza."

Kerumbo alikiri kwamba tayari amepata mtoto mmoja katika ndoa yake ya sasa.

"Niko na mtoto mmoja. Sijui kama atakubali nikuje na huyo mtoto. Nitarudi kwa sababu niko na watoto naye," alisema.

Kerumbo alidai kwamba alimtema Bw Julius kwa sababu alikuwa akienda nje ya ndoa sana.

"Niliona badala aniletee magonjwa nikufe niache watoto, ni heri niende," alisema.

Julius alimwambia, "Ata kama makosa ilipatikana mimi bado nakupenda, urudi tuendelee na maisha."

Kerumbo hata hivyo alimtaka mume huyo wake wa zamani asiulize maswali mengi wakati atakaporudi kwani yeye ndiye alikosea.