Mwanamume ataka kurudiana na mke hata baada ya kudai kumkuta kwa nyumba ya jamaa

Samwel Wafula alisema kwamba bado anampenda mke wake Naliaka kama kiti moto!

Muhtasari

• Alisema alijificha na kumuona mke wake akitoka kwa nyumba ya kijana huyo usiku na kunyata kwenda kwa nyumba yao.

• Alipomfuata mwanamume yule na kumuuliza, aliambiwa kuwa mkewe hakuwahi sema ana mume.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Mwanamume mmoja kwa jina Samwel Baraza alipeleka ombi la kutaka kupatanishwa na mke wake Naliaka ambaye alitoroka nyumbani baada ya kumfumania na mwanamume jirani yake.

Kwa maelezo ya Samwel katika kipindi cha Patanisho na Gidi na Ghost, alisema kwamba Naliaka anamshinda kwa miaka miwili na alimuoa akiwa na mtoto mmoja kabla ya kuongeza mtoto mwingine na yeye.

Samwel alisema kuwa Naliaka kumuacha kwa miaka miwili hakujawahi kuwa tatizo .

Lisimulia kilichotokea mpaka kutengana na mke wake, kuwa alitoka kwa nyumba kwenda kutafura nauli ya kusafiri kwenda kwao nyumbani kwa ajili ya mazishi, hapo ndipo pia mke wake alipata mwanya wa kutoka pasi na kumjulisha Samwel.

“Ilikuwa juzi nilikuwa na mazishi nyumbani  nikatoka kwenda kutafuta nauli na kumuacha kwa nyumba, kumbe pia yeye akatoka nikashindwa ameenda wapi…… kumpigia simu hataki kushika ikabidi nikaeka simu yangu private ndio labda anaeza shika…. Msichana mwingine akashika akaniambia ni dada yake,” Samwel alieleza.

Alisema kwamba ushawishi wa huyo mwanadada mwingine kujiita dadake haukumuingia na kutokana na wasiwasi, alikesha kwa lango la boma ambayo walikuwa wamekodisha hadi giza. Hapo ndipo alimuona mke wake akinyata kutoka kwa nyumba ya jamaa mmoja aliyekuwa akiishi hapo, akaelekea kwa yule msichana na kuchukua mtoto kabla ya kurudi kwa nyumba yao – bila kujua kama mume wake alikuwa anamuangalia kutoka sehemu alikokuwa amejificha.

“Nikaenda kwa huyo jamaa kumuuliza anafanya nini halafu akaniambia mke wako aliniambia hana mwanamume,” Samwel alisema.

Aliamua kurudi kwa nyumba yake kumuuliza mke wake kile alichoshuhudia na mke wake alikurupuka na kutoroka nje akiambia majirani kwamba amefukuzwa. Alipiga kelele akitaka kuruhusiwa kupewa mtoto na akaondoka kwenda zake.

Licha ya visanga hivyo vyote, Samwel bado alisisitiza kwamba anampenda mke wake na alitaka kurudiana naye.

Kwa upande wake Naliaka alisema ako radhi kurudiana na Samwel lakini kwa sharti kwamba hawezi kurudi kule walikokuwa wakiishi awali.

Pia alikanusha madai ya Samwel kuwa alienda kwa mwanamume mwingine na kusema kwamba alienda kwa dadake kutokana na Samwel kumfukuza mara kwa mara usiku wa manane.

“Ananisingizia vitu ambavyo sijafanya. Mimi nina mtoto wa miezi 4 na siwezi kuwa naenda na wanaume wengine kimapenzi,” Naliaka alisema.

Alimtaka Samwel kutafuta nyumba sehemu tofauti au kuhamia kwa nyumba ambayo anaishi, lakini Samwel akakataa akisema kwamba hawezi ishi kwa nyumba ya mwanamke ambaye hajui kama ni mwanamume analipa kodi.