Patanisho: Mama mkwe amlaani mjukuu wake baada ya mwanadada kukataa kurudiana na mwanawe

Oroni alisema mkewe alimdanganya kwamba ameenda matanga na amekataa kurudi.

Muhtasari

•Oroni alidai kwamba mkewe hajampatia sababu yoyote ya kukataa kurudi kwa ndoa ya ya miaka mitatu.

•Mama Sharvin alidai kuwa mama mkwe wake alimlaani mtoto wao baada ya yeye kukataa kurudi kwa ndoa yao.

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Boniface Oroni alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Mama Sharvin ambaye alienda nyumbani na hajawahi kurudi.

Oroni alisema kuwa mke wake alimwambia kuwa alikuwa na matanga ya kuhudhuria nyumbani kwao Uganda ila amekataa kurudi.

"Aliniambia kwao kuna matanga nimtafutie nauli. Nilimtafutia akaenda. Bado hajarudi. Kila mara anasema yuko tayari kurudi, natuma nauli lakini hakuna dalili. Juzi nimemtumia pesa nzuri, bado hakuna dalili," alisema.

Oroni alidai kwamba mkewe hajampatia sababu yoyote ya kukataa kurudi kwa ndoa ya ya miaka mitatu.

"Tuliongea na mama yake. Aliniambia niende kwao nyumbani. Nilimwambia nitaenda mwezi wa sita. Bado sijalipa mahari. Mimi najua ni matanga ilifanya akaenda. Kama nilikosea naomba aniambie," alisema.

Mama Sharvin alipopigiwa simu alifichua kuwa Oroni alimtunga mimba mwanadada mwingine ambaye alimfanya amweke pembeni.

"Huyo jamaa alikuja akawa na msichana huko nje ambaye alipea mimba. Alikuwa akitoka kwa nyumba anarudi usiku saa saba, saa nane, saa tisa. Nilichoka. Nikimwambia anipatie nauli niende alikuwa anakuwa mkali," Mama Sharvin alisema.

Aliongeza, "Nilimdanganya kuna matanga nyumbani akanitafutia nauli. Nilimwambia mimi sirudi  alete huyo msichana ambaye huwa anafanya arudi kwa nyumba usiku. Alinibembeleza mimi nikakataa."

Mama Sharvin alidai kuwa mama mkwe wake alimlaani mtoto wao baada ya yeye kukataa kurudi kwa ndoa yao.

"Kukataa, mama yake akaanza kulaani mtoto wangu kwa simu. Kutoka wakati huo mtoto amekuwa mgonjwa."

Mama Sharvin hata hivyo alidokeza kuwa yuko tayari kurudi iwapo mumewe atarekebisha tabia zake mbaya.

"Hiyo miaka yangu si ya kuniacha kwa nyumba usiku. Mimi ameniweka kama ng'ombe ambaye ataletea maji na majani,"

Oroni alimuomba radhi mkewe kwa mienendo yake mibaya na kuahidi kuwa mume mwema wakati wakirudiane.

"Baridi inanipiga kwa sababu hauko. Msichana huyo mwingine alienda kwao. Sijawahi kuenda kwao saa nane. Huwa natoka kazini," Oroni alimwambia mkewe.

Mama Sharvin aliahidi kurudi na kumhakikishia mumewe kuhusu upendo wake kwake.

"Nakupenda kama mume wangu na baba wa watoto wangu. Ukibadilika nitarudi," alisema.