Patanisho: Kijana amtusi na kumpiga babake baada ya kukataa kumgawia shamba

"Alikataa ikafanya nipandwe na hasira nikamtusi. Nilikasirika zaidi hadi nikamchapa kidogo," alisema

Muhtasari

•Bw Oscar alisema mzozo wao ulitimbuka baada ya mzazi huyo wake kukataa ombi lake la kugawiwa shamba.

•Oscar alimuomba mzazi huyo wake kukubali ombi lake la msamaha huku akimthibitishia kwamba amejuta.

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Oscar Juma ,23, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na babake James Juma, 48, ambaye alitofautiana naye mwaka jana.

Bw Oscar alisema mzozo wao ulitimbuka baada ya mzazi huyo wake kukataa ombi lake la kugawiwa shamba.

"Nilitaka anigawie shamba. Nikawa nabishana naye. Alikataa ikafanya nipandwe na hasira nikamtusi. Nilikasirika zaidi hadi nikamchapa kidogo," alisema.

Aliongeza, "Nilimchapa kwa sababu aliniambia hata anaweza kataa kunigawia shamba. Nawanga na hasira sana. Nilikuwa nataka kutoka kwa Simba nijenge kwangu.Aliniambia nisiwe na haraka eti akitaka kugawa shamba ataniambia."

Juma alisema baada ya kuzozana na babake alitoroka nyumbani na kuenda Kiambu ambako amekuwa akifanya kazi ya mjengo.

"Sasa huwa hashiki simu. Nataka niombe msamaha ili nirudi nyumbani," alisema.

Bw James alipopigiwa simu alithibitisha kuwa alizozana na mwanawe baada ya kumshinikiza amgawie shamba. Alidokeza kuwa Oscar alikuwa chini ya shinikizo la marafiki wabaya ambao walimshauri kudai shamba.

"Oscar ni kijana yangu. Ni vizuri kama amekaa chini na akafikiria makosa yake. Ni kijana mdogo lakini alikuwa anadai shamba wakati ambao sijafikia kumpatia shamba. Ni mambo tu na makundi mbaya mbaya lakini sio kupenda kwake. Mtoto kama huyo ukimgawia shamba sasa hivi si ataenda kuuza?!" alisema.

Oscar alimuomba mzazi huyo wake kukubali ombi lake la msamaha huku akimthibitishia kwamba amejuta.

"Ningependa kukuomba msamaha kwa kukutusi na kukuchapa," alisema.

Bw James aliweka wazi kwamba tayari amemsamehe mwanawe ila akamwagiza afunge safari ya nyumbani ili wasuluhishe kabisa.

"Kuna utaratibu wa kuomba mzazi msamaha. Afunge safari akuje nyumbani aombe msamaha. Akuje nyumbani tukae chini kama familia tuzungumze ili maisha yake yanyooke," James alimwabia mwanawe.

Oscar alisema ataenda nyumbani mwezi wa nane baada ya kufanya kazi na kukusanya fedha za kutosha.

"Wakati wowote ukipata nafasi ukuje," babake alimwambia.

Je, una maoni yepi kuhusu Patanisho ya leo?