"Nimeacha kuhanyahanya, nimeokoka Yesu ni Bwana!" Jamaa ajinyenyekeza akimsihi mke arudi

Makokha alisema siku hizi huwa anaenda kanisa na hata ameweza kununua Bibilia.

Muhtasari

•Makokha alisema ndoa yake ya miaka miwili ilivunjika Agosti mwaka jana baada ya yeye kucheza karata nje ya ndoa.

•Mwende alikubali kumsamehe mumewe na kurudi huku akieleza matumaini kwamba ameweza kurekebika.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, Sammy Brian Makokha kutoka Bungoma  alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Winnie Mwende.

Makokha alisema ndoa yake ya miaka miwili ilivunjika Agosti mwaka jana baada ya yeye kucheza karata nje ya ndoa.

Alikiri kuwa alikuwa na mazoea ya kutaniana na wanawake wengine katika kilabu baada ya kubugia mvinyo.

"Nilikuwa na bibi yangu. Nikawa nahanyahanya wanadada wengine huko nje. Nilikuwa nahanya kwa klabu wakati nimelewa," alisema.

Aliongeza "Nilijaribu kumwambia aka echini tuongee lakini akasema anataka kuenda kwao. Mimi sikuwa na ubaya, ni shetani alinifanya nikawa nahanyanya.  Nimeongea na baba yake akasema niende nyumbani tuongee."

Makokha alisema ingawa amekuwa akizungumza na mkewe, bado hajaweza kukubali ombi lake la kurudiana. Hata hivyo, alitoa hakikisho kwamba tayari amejirekebisha na hata kuchukua hatua ya kuokoka.

"Nilizaa na yeye mtoto mmoja lakini alikuwa amekuja na mwingine. Alienda na watoto wote nikaachwa pekee yangu kwa nyumba.  Nimeacha kuhanyahanya siku hizi, nimeokoka Yesu ni Bwana.Hata nilikuwa na uwongo mwingi lakini nimekubali kutulia kabisa nishughulikie familia yangu." alisema.

Mwende alipopigiwa simu alithibitisha kuwa alimtema mzazi huyo mwenzake kwa tabia yake ya kuenda nje ya ndoa na kulewa. Alisema aliondoka ili kumpatia mumewe muda wa kurekebisha mienendo yake mibaya.

"Niliamua kumpatia muda abadilike kwa sababu nilijaribu kuongea na yeye akakataa. Nilijaribu hata kuongea na mzazi wake lakini hakusikia. Kuhanyahanya na kulewa ndiyo ilifanya nikatoka," alisema Mwende.

Makokha alimuomba msamaha mkewe na kumhakikishia kwamba amerekebisha tabia zake.

"Nimeacha pombe hata wasichana nimeacha. Nina uhakika sitawahi kurudia," alisema.

Mwende alikubali kumsamehe mumewe na kurudi huku akieleza matumaini kwamba ameweza kurekebika.

"Nimekubali kurudi kama amebadilika. Siku hizi hata siamini. Vile anaongea ni kama amebadilika. Kitambo hakuwa hivyo lakini siku hizi hata mambo ya Mungu anajua," alisema.

Makokha alisema siku hizi huwa anaenda kanisa na hata ameweza kununua Bibilia ambayo amekuwa akisoma mara kwa mara.

"Babe aakupenda kama supu ya Omena. Wewe ni mama ya watoto wangu. Hakuna vile nitaoa mwanamke mwingine nimlete kwa nyumba. Nimeangalia nikaona wewe ndiye unanifaa," alimwambia mkewe.

Mwende alisema, "Makokha pia mimi nakupenda na ningependa turudiane. Mambo ya kuhanyahanya uache. Turudiane tuendelee na maisha."