Patanisho:"Sikupendi! Enda umuoe Sylvia!" mwanadada amwambia mumewe, akiri kula fare

"Mimi nishamove on. Siwezi nikarudi," Eunice alisema.

Muhtasari

•David alisema ndoa yao ya miaka mitatu iligonga ukuta baada ya mkewe kuenda nyumbani kwao kwa ajili ya matanga na kukosa kurudi.

•Eunice aliweka wazi kwamba mzazi huyo mwenzake hajakuwa akishughulikia mtoto wao wa miaka mitano.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

David Khaemba kutoka Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mke wake Eunice ambaye alitengana naye Desemba 2021.

David alisema ndoa yao ya miaka mitatu iligonga ukuta baada ya mkewe kuenda nyumbani kwao kwa ajili ya matanga na kukosa kurudi.

"Tuliona 2018. Tulikaa kwa ndoa miaka 3. Desemba 2021 alisema kuna matanga kwao na wanamhitaji. Nilimtafutia nauli akaenda," alisimulia.

Aliongeza, "Matanga ilipoisha, alisema ati nimtumie nauli tena kwa kuwa amemaliza pesa zote. Nilitafuta pesa na nikamtumia. Lakini hadi wa leo hajawahi kuja."

David alisema kuwa alizungumza na mzazi huyo mwenzake wiki iliyopita na akaahidi kurudi iwapo angetuma nauli. Hata hivyo, alihofia kutuma pesa zozote kwa kuwa alihisi kama kwamba mkewe huyo wa zamani alikuwa anamchezea.

"Alikuwa anasema kama sitaachana na mambo ya pombe hatawezana na mimi. Nilimwambia kama ni kurudi nitaacha pombe kidogo kidogo tu. Naacha pombe polepole. Nikisema nimeacha nitakuwa nafanya ukora," alisema.

Jamaa huyo alisema kwamba angetaka kujua msimamo wa Eunice kwa kuwa wametangana kwa muda mrefu.

Mtangazaji Gidi alipompigia simu Eunice, aliweka wazi kuwa tayari amesonga mbele na maisha yake na kubainisha kwamba hakuna uwezekano wa kurudiana na baba huyo wa mtoto wake mmoja.

"Mimi nishamove on. Siwezi nikarudi," alisema.

David alimwambia, "Mimi nakupenda kabisa. Badilisha huo msimamo. Maji naacha polepole, sijaacha kabisa."

Eunice aliweka wazi kwamba mzazi huyo mwenzake hajakuwa akishughulikia mtoto wao wa miaka mitano.

Aidha, alifichua kwamba David alikuwa na tabia ya kuhanyahanya na hata aliwahi kuoa mwanadada mwingine kwa jina Sylivia.

"Enda umtafute Sylvia umuoe. Wewe endelea na maisha yako mimi nishamove on," alimwambia David.

Alisema, "Huyo mwanaume alinipigia simu nikaacha kazi nikarudi kwake. Kufika huko ata sikukaa .Wasichana ako nao wengi.Alikuwa anabebwa na bosi wake kupelekwa klabu. Baadaye napigiwa simu nimuendee akiwa amelewa chakari. Pombe anakunywa, sigara na bangi pia anavuta. Mimi nilishatafuta kazi, nikamove on, naendelea na kazi yangu, nitapata bwana mzuri wa kunioa,"

Eunice alikiri kwamba alikuwa nauli mara mbili baada ya mumewe huyo wa zamani kumtumia ili arudi. 

David alimwambia, "Mimi nakupenda kama bibi wangu wa kwanza. Yale nilikufanyia nimekusamehe. Tafadhali rudi tukae."

Eunice hata hivyo alijibu,"Wewe tafuta msichana ambaye anaweza kuvumilia tabia zako umuoe. Sikupendi!"