Patanisho: Jamaa ampiga mkewe hadharani wakielekea kanisani

Clinton alikiri kwamba ilikuwa mara ya pili kwa yeye kumpiga mkewe.

Muhtasari

•Clinton alisema alikasirika na kumpiga mkewe baada ya kumjibu vibaya alipomuuliza kuhusu shati lake pendwa la kuenda kanisa.

•"Nakupenda sana. Hakuna kitu naweza kufananisha nawe. Nakupenda kama vituko vya Yesu wa Tongaren," Clinton alimwambia mkewe.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Clinton Keith kutoka Vihiga alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Marlin Lokela ambaye alikosana naye Jumapili baada ya kumzaba kofi.

Clinton alisema alikasirika na kumpiga mkewe baada ya kumjibu vibaya alipomuuliza kuhusu shati lake pendwa la kuenda kanisa.

Hata hivyo alisema kuwa anajutia kitendo chake na kuomba asaidiwe kurudiana naye.

"Siku ya Jumapili asubuhi nilimuuliza shati iko wapi. Akasema ‘Aah, wacha kunisumbua’ nikakasirika nikamchapa kofi. Hata mimi sijui vile nilimchapa kofi. Nilishtukia tu. Alilia, nikamtuliza alafu tukaenda kanisan. Nadhani nilimkosea. Sasa hivi amenyamaza tu, sijui anapanga vipi," alieleza.

Clinton alikiri kwamba ilikuwa mara ya pili kwa yeye kumpiga mkewe.

Marlin alipopigiwa simu alieleza matukio yaliyotokea siku ya Jumapili.

"Yeye aliniuliza hiyo shati iko wapi. Hapo awali, yeye mwenyewe alikuwa amesema akiamka atajua shati atavaa. Nilimuwekea shati mbili hapo. Wakati alipotoka bafu nilimwambia kuna shati mbili hapo kwa kiti ajue yenye atavaa. Katika harakati hizo akanipiga kofi, mimi nikanyamaza tu," alisimulia.

Aliendelea, "Nilisema sitaenda kanisa kwa sababu ameniharibia mood. Ata yeye akakataa kuenda. Baadaye akabadilisha msimamo akasema ataenda. Hapo kulikuwa na mtoto wetu mmoja wa miaka 12, alianza kumueleza jinsi amenipiga kofi kwa sababu ya shati. Mtoto alimwambia hayo ni maneno yetu."

Marlin alifichua kwamba mumewe alimpiga kofi tena na kumtusi hadharani walipokuwa wakielekea kanisani

Clinton alikiri makosa yake na kumuomba radhi mzazi huyo mwenzake.

"Marlin unajua vile nakupenda. Nakuomba unisamehe tu. Hata mimi naskia uchungu kwa yale nilitenda," alisema.

Marlin aliweka wazi kwamba hana shida yoyote na mumewe ila akamsihi abadilishe mienendo yake. Pia alipuuzilia mbali wasiwasi wa Clinton kwamba alikuwa na mipango ya kutoroka.

"Kabla tuende kanisa nilimwambia nataka kuenda. Aliniambia niende. Aliniambia nikitaka kulia nilie nikitulia ninyamaze," alisema.

Clinton alimhakikishia mkewe kuhusu upendo wake mkubwa kwake na kuahidi kurekebisha tabia zake.

"Nakupenda sana. Hakuna kitu naweza kufananisha nawe. Nakupenda kama vituko vya Yesu wa Tongaren. Huwa ananifanya nafurahia sana," alisema.

Marlin alisema, "Nimekubaliana na yeye vile amesema. Sina mtu mwingine kando yake. Badilika ama utakuja kunipoteza."