Jamaa aliyejitambulisha kama Eric Kamanda ,35, kutoka Narok alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mke wake Sophie Nyambeta ,29, ambaye alitengana naye takriban miaka miwili iliyopita.
Eric alisema ndoa yake ya miaka 5 ilivunjika baada ya mkewe kushindwa kugharamia matibabu ya mkewe alipougua.
"Nilioa mwaka wa 2016 lakini tumesumbuana na mke wangu. Tumesumbuana na baba, mama mkwe na jamaa zake wake," Eric alisimulia.
Aliendelea, "Nilipata shamba Narok. Wakati moja tulikuwa tunalima akajikata mguu, sikuwa na pesa za kumpeleka hospitali, nikaomba kwa kaka yake. Nilipompeleka hospitali, hakupona kwa sababu daktari alimfunga vibaya. Sikuwa na uwezo wa kumlipia matibabu zaidi akaanza kuomba watu wa kwao wamsaidie. Walimtumia nauli akaenda. Alinidanganya anaenda kutibiwa nyumbani lakini hakuenda. Alienda kukaa kwa shangazi yake akatibiwa."
Alifichua kwamba alijaribu kumtafuta mkewe na wakati alipomtembelea nyumbani kwa shangazi yake alipigwa hadi kutoroka.
"Mimi nilienda kwa shangazi lakini wakati aliniona akajifungia kwa nyumba. Shangazi yake alipokuja alichukua rungu akanipiga na kuniumiza mkono. Nilitoroka nikaenda nyumbani. Nilieleza mama yangu na wanafamilia kadhaa tukaenda kwao. Baba yao alisema wako safarini na kuzima simu," Eric alisema.
Eric alisema hakufa moyo na alifanya ziara nyingine nyumbani kwa kina mkewe ila yeye na wageni wake hawakuwahi kupokelewa.
"Babake alitufukuza na wazee wakati tulienda kwao mara nyingine. Alitupatia dakika mbili tupotee. Nimeenda huko mara mbili. Mke wangu alianza kunitafuta mwezi wa tatu mwaka huu.. Alitoka akaenda Kisumu. Sasa hivi ako Nyamira. Nampenda mtoto wangu sana. Nataka nimuombe msamaha. Nataka familia yangu," alisema.
Sophie alipopigiwa simu alimlalamikia mzazi huyo mwenzake kwa kumtusi mzazi wake. Pia alimweleza Eric kwamba tayari amesonga mbele na maisha yake na kumshauri atafute mwanamke mwingine wa kuoa.
"Kwa nini unatusi wazazi wangu? Kwa nini unasema maneno mabaya kwa baba yangu? Unamwambia sitawahi kuoelewa?" Sophie alilalamika.
Aliendelea, "Mimi nimeshamove on, pia wewe move on. Mimi nilikuwa rafiki wako tu. Kama tulikosana mimi na wewe, baba yangu anaingilia wapi?"
Sophie aliendelea kusema, "Kuna ujumbe alitumia baba yangu akamwambia anajifanya ni deacon wa kanisa na hawezi kusameheana. Alikuwa ameniambia ati nilitoka kwake na mimba nikaenda nikatoa. Akaniambia ati hata mtoto ambaye niko na yeye nikiona ni mzigo kwangu hata yeye nimuue."
Eric alisema anajuta matendo yake ambayo alisema yalitokana na hasira kubwa ambayo alikuwa nayo moyoni mwake.
Alidai kwamba baba mkwewe tayari alikuwa amekubali kumsamehe ila baadaye akageuza msimamo wake na kumtusi.
Sophie alisema, "Hajawahi kusaidia mtoto hata kitu, ndio maana babangu ako na machungu. Ndio maana baba yangu alimuuliza anasema yeye ni baba nani. Mimi nimeshaamua komove on na maisha yangu. Hata nikiwa kwake nilikuwa napitia maisha magumu. Sitaki kurudiana na yeye."
Eric alijaribu kumshawishi mkewe atulize moyo wake na kukubali kurudiana.
"Siwezi kumsahau na siwezi kusahau mtoto wangu. Nimejaribu mambo mengi lakini nitaachia tu mwenyezi Mungu," alisema.
Huku akimjibu, Sophie alisema, "Hata mimi nakutakia maisha mema. Umove on, hata mimi nimemove on maisha yangu."
Eric hata hivyo aliendelea kujitetea huku akimwambia mzazi huyo mwenzake, "Ningependa unipatie nafasi ya mwisho. Nimejirekebishia. Nilijiheshimu nikasema niko na familia."
Huku kitengo cha Patanisho kikikaribia kuisha, Sophie alifunguka mambo zaidi kuhusu mume huyo wake wa zamani akisema, "Hajawahi kunilipia hata mahari. Nilikuwa na moyo wa kurudi lakini vile alianza kutusi wazazi wangu ilianza kuniuma. Kitu ilinitoa kwake ni bangi. Alikuwa anavuta bangi alafu akikuja kwa nyumba anaanza kubishana na mimi. Mimi nimeshamove on."
Je, maoni yako ni yapi kuhusu Patanisho ya leo?