Patanisho: Jamaa alalamika kuhusu mkewe kutaka msamaha bila kukiri makosa yake

"Kuna uwezekano wa kurudiana lakini ni kitu ingine ngumu sana. Itahitaji kufanyiwa vitu nyingi lakini inawezekana," Kinoti alisema.

Muhtasari

•Kendi alisema ndoa yake ya miaka minne ilisambaratika mwezi Machi mwaka jana kufuatia mizozo ya kinyumbani.

•Kendi aliendelea kujitetea kwa mzazi huyo mwenzake huku akimuomba ampe nafasi ya mwisho na kuahidi kubadilika.

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Carol Kendi ,29, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Harrison Kinoti ,28, ambaye alitengana naye mwaka jana.

Kendi alisema ndoa yake ya miaka minne ilisambaratika mwezi Machi mwaka jana kufuatia mizozo ya kinyumbani.

"Ilikuwa mambo ya kutoelewa nyumbani. Mimi niliona ni kama hataki pale nyumbani. Alikuwa ananiambia ata nikitoka hawezi kusikia kitu. Mimi nikaona ni kama hanitaki nikaenda. Nilitoka nikaenda na mtoto," Kendi alisimulia.

Aliongeza, "Hapo awali nilikuwa nampigia ananitusi. Kufika mwezi wa tisa mwaka jana alianza kunipigia akasema ningerudi mwezi wa kwanza. Kufika akasema ningerudi mwezi wa tatu, kufika mwezi wa tatu akanyamaza kabisa."

Harrison alipopigiwa simu alisikika kushangazwa sana na hatua ya mzazi huyo mwenzake kuleta kesi yao katika Patanisho.

Kendi alichukua fursa hiyo kuomba msamaha na kumhakikishia mumewe kuhusu mapenzi yake mazito kwake.

"Kama nilikukosea unisamehe. Sijui ni kosa gani nilifanya huwezi kunisamehe. Nimeona nikupeleke Radio Jambo ndio ujue nakupenda," Kendi alimwambia mumewe.

Harrison alisema, "Hiyo mambo ni ngumu sana. Kuna vitu zingine siwezi kuambia kwa hewa. Ndio maana nashangaa sana amekumbuka aje. Wacha anipigie simu tuongee."

Hata hivyo, alidokeza kwamba kuna dalili ya wao kurudiana.

"Kuna uwezekano wa kurudiana lakini ni kitu ingine ngumu sana. Itahitaji kufanyiwa vitu nyingi lakini inawezekana," alisema.

Aliongeza, "Shida na wasichana wakifanya makosa wanafanyanga vitu vingine wakifikiria ni sawa lakini hawaoni kama ni makosa. Mtu akifanya makosa alafu anataka kusamehewa lakini inakuwa ngumu sana kukiri makosa ni kujitetea tu sio sawa. Mimi sio mtu wa kupiga kelele Huwa hakubali makosa."

Kendi aliendelea kujitetea kwa mzazi huyo mwenzake huku akimuomba ampe nafasi ya mwisho na kuahidi kubadilika.

Harrison alisema, "Naweza kumpatia nafasi nyingine lakini sio kwa haraka, anipatie wiki moja .Anipigie simu tutazungumza."

Wawili hao walikubaliana kuzungumza baadaye na kujaribu kusuluhisha mzozo wao.