Patanisho: Mwanadada akasirika, aandika ‘siku sitawahi sahau’ baada ya mumewe askari kutuma picha yao kwa rafiki

Gilbert alisema mkewe hakupendezwa na kitendo chake kutuma picha kwa rafikiye na mara moja alianza kugombana naye.

Muhtasari

•Gilbert alisema mke wake wa mwaka mmoja amekuwa akimshuku kuwa na mahusiano ya nje na wamekuwa wakizozana kwa hilo.

•Everlyne alimtaka Gilbert kuacha kisirani na kuwa mwaminifu kama jinsi yeye alivyodai kuwa mwaminifu.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Afisa wa polisi, Gilbert Kiprotich (31) kutoka Eldoret alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Everlyne Lideva (31) ambaye alikosana naye takriban wiki moja iliyopita kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Gilbert alisema mke wake wa mwaka mmoja amekuwa akimshuku kuwa na mahusiano ya nje na wamekuwa wakizozana kwa hilo.

"Bibi yangu anafanya kazi Muthaiga. Nikienda nyumbani huwa ananishuku. Nikienda nyumbani huwa namuuliza tufanye aje kwa maisha. Nikienda huwa ananiuliza mahali niliko nimezaa watoto wangapi. Mimi huwa nanyamaza kwa sababu sitakangi maneno," Gilbert alisimulia.

Aliendelea, "Wiki jana nilimtembelea mahali anaishi. Kufika tukaongea. Siku nilifaa kuenda kazi nilipoamka kuna rafiki yangu aliuliza niko wapi nikamwambia niko nyumbani na nikamtumia picha kumthibitishia. Bibi yangu alikuja akachukua simu akaona ile picha alafu akaamka akaenda hadi kwa kalenda akaandika "siku ambayo sitawahi kusahau'. Bado sijujua ama ni hii picha hakutaka nitume ama alikuwa na maneno na huyo rafiki yangu."

Gilbert alibainisha kuwa mkewe hakupendezwa na kitendo chake kutuma picha kwa rafikiye na mara moja alianza kugombana naye.

Everlyne alipopigiwa simu alibainisha kuwa alikuwa na sababu zake kuandika kwa kalenda baada ya kuzozana na mumewe.

Aidha alimtaka Gilbert kuacha kisirani na kuwa mwaminifu kama jinsi yeye alivyodai kuwa mwaminifu.

"Aache kisirani, aanze kuwa mwaminifu juu mimi ni mwaminifu na simu yake. Simu yake huwa anaweka password, inafika mahali anazima. Hakuna kuficha, sina shida na yeye, nampenda sana," Everlyne alisema.

Gilbert alisema suala la kisirani ni jambo ambalo anaweza kudhibiti.

Pia aliahidi kuwa mwaminifu na kuwa anampa mkewe simu yake wakati akienda nyumbani.

"Nitajaribu. Nikitoka kazini sio vizuri mtu kushika simu yangu. Nikirudi hiyo password nitatoa," Gilbert alisema.

Everlyne pia alimwagiza mumewe kupeleka mahari nyumbani kwao akisema, "Huwezi kusema unanipenda na hujapeleka mahari. Hiyo akitimiza tuko tu sawa. Kwa sababu mtu mwingine akitaka kunichukua na hujatoa mahari atanichukua."

Gilbert aliahidi kutoa mahari kwa ajili ya mkewe kufikia mwisho wa mwaka huu.

"Everlyn mimi nakuhakikishia nakupenda sana . Nakupenda kama kazi yangu ambayo nafanya," alimwambia Everlyne.

Everlyne pia alimhakikishia mumuwe kuwa anampenda na kumheshimu sana.