Patanisho: Jamaa asononeka baada ya kuachwa kutokana na ulevi, uasherati, kumpiga mkewe

Kerubo aliweka wazi kwamba hataki mambo ya mume huyo wake tena na kumwagiza aendelee na maisha yake.

Muhtasari

•Momanyi alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka mitatu kutokana na tabia yake ya ulevi na vurugu kwenye nyumba.

•"Anafanya kazi lakini pesa inaenda kwa pombe na uasherati, tena sio mbali.  Alafu analeta hadi kwa nyumba yangu," Kerubo alilalamika.

Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Adamson Momanyi ,26, kutoka Kisii alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Catherine Kerubo ,24, ambaye alimuacha takriban wiki mbili zilizopita.

Momanyi alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka mitatu kutokana na tabia yake ya ulevi na vurugu kwenye nyumba.

"Nilikuwa nakunywa pombe na mke wangu alikuwa ananikataza siskii. Mimi nilikuwa nakunywa, nikiingia kwa nyumba tunazozana inaleta hasira, alikuwa akinigombeza akiniambia alinikataza kunywa pombe. Kufuatia hayo, mimi nilikuwa namtusi namalizia kumchapa. Najuta sana juu nimeteseka sana. Nimebadilika," Momanyi alisema.

Alidai kwamba hajaonja pombe hata kidogo katika kipindi cha wiki mbili zilizopita tangu mkewe kuondoka nyumbani.

"Nimeacha kabisa. Ilikuwa mambo na marafiki. Nimeachana nao. Pombe ndio ilikuwa inafanya nimpige. Akiniambia nilikuwa naona kama ananiambia vibaya. Hapo awali nilikuwa nampigia simu anachukua. Wakati nilimwambia niende tuongee na yeye, aliniambia hawezi kuongea na mimi hadi nibadilike," alisema.

Alikiri kwamba alimkosea sana mkewe wakati alipoamua kutoroka na kudai kwamba tayari amebadilika kabisa.

Kerubo alipopigiwa simu, aliweka wazi kuwa hataki kuzungumza na mzazi huyo mwenzake na kukata simu mara moja.

"Mimi sitaki," alisema.

Momanyi alisema, "Amenikataza pombe siku nyingi. Sijui shida ni nini aki.. Mimi nimeachana na pombe kabisa."

Baada ya Gidi kumpigia tena Kerubo, aliweka wazi kwamba hataki mambo ya mume huyo wake tena na kumwagiza aendelee na maisha yake.

Kerubo alifunguka kuhusu baadhi ya masaibu ambayo alikuwa anapitia akiwa na mzazi huyo mwenzake.

"Aendelee na maisha yake. Mimi sitaki mtu wa kunipiga kila mara. Pia kazi hataki kufanya chochote. Anaenda kufanya hiyo kazi lakini pesa inaenda kwa pombe na uasherati, na sio mbali hapo tu karibu na kwangu.  Alafu analeta hadi kwa nyumba yangu. Sitaki stori zake kabisa. Aache mimi nifanye kazi," Kerubo alisema.

Aliongeza, "Hadi mamangu akimuuliza anatusi mama yangu na watu wangu, akiulizwa anasema ni pombe. Sitaki mambo yake kabisa."

Momanyi alipojaribu kuomba radhi na kumuita mkewe majina matamu, Kerubo alimwambia, "Usijaribu kuniita hivyo, am not your babe for now. Ulikuwa unanipiga alafu unadanganya mama yangu na mimi nimelala kitandani. Achana na mimi tafadhali."

Momanyi alimwambia, "Pole mami, walai sitawahi kurudia. Nimebadilika, hadi nimekonda. Mimi nakupenda.Nakusihi urudi tulee mtoto. Mimi sitawahi kukupiga tena. Ata nikikunywa nitakuwa naingia tu kwa nyumba nalala. Sioni kama nitaishi kwa hii maisha bila wewe. Kuja tulee mtoto wetu pamoja."

Je, una ushauri gani kwa wawili hao?