Patanisho: Wafula afurahia chakula kilichopikwa na mkewe kabla ya kugundua ametoroka na vitu vyake

Wafula alifichua kuwa wakati mkewe alitoroka alimuacha mtoto ambaye alizaa naye kwa jirani yao.

Muhtasari

•Wafula alisema haelewi kilichomfanya mkewe kugura ndoa yao ya miaka miwili ila akadokeza alikuwa anamshuku kuwa na mpango wa kando.

•Wafula alisema siku mkewe alitoroka, mwanzoni hakudhani kuna chochote kibaya kimetokea hadi alipogundua nguo zake haziko.

Image: RADIO JAMBO

Josphat Wafula ,24, kutoka Turbo alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Purity Wamalwa ,23, ambaye alitoroka hivi majuzi.

Wafula alisema haelewi kilichomfanya mkewe kugura ndoa yao ya miaka miwili ila akadokeza alikuwa anamshuku kuwa na mpango wa kando.

"Tulioana 2021. Nilimuoa na mtoto mmoja alafu tukapata mtoto mmoja.Amekuwa ananishuku niko na mpango wa kando, lakini sina," Wafula alisimulia.

Aliendelea, "Nilikuwa natoka kazi jioni nikapata hakuna vitu vyake kwa nyumba. Nilipata supper imeundwa vizuri lakini na mlango imefungwa. Kuingia kwa nyumba sikumuona nikadhani ako kwa jirani. Nikakula supper yangu vizuri alafu nikaelekea kwa malazi, hapo ndipo nikaona hakuna vitu zake kweli. Kujaribu kumpigia simu hakuchukua. Nikajaribu tena na tena mpaka akaniblock. Hadi sasa ameniblock"

Wafula alisema siku mkewe alitoroka, mwanzoni hakudhani kuna chochote kibaya kimetokea hadi alipogundua nguo zake haziko.

"Mimi sikuwa nashuku chochote. Nilipata mlango imefungwa na funguo imewekwa mahali huwa tunaweka. Kuenda kuangalia manguo yake niliona hakuna. Sijajaribu kuongea na wazazi kwa sababu niko na namba yake tu," alisema.

Juhudi za kumpatanisha Wafula na mkewe kwa bahati mbaya ziligonga mwamba kwani Purity hakuchukua simu alipopigiwa.

Wafula alifichua kuwa mwanadada huyo alipotoroka alimuacha mtoto ambaye alizaa naye kwa jirani yao.

"Watoto aliacha mmoja, aliacha yule wangu akaenda na mmoja. Alimuacha kwa jirani tu.Nilikuwa napenda watoto wote. Nikileta switi napatia wote," alisema. 

Aliongeza, "Kuna siku timu ya Arsenal ilikuwa inacheza. Nikaenda kutazama. Kwa bahati mbaya nikachelewa. Alisema nilikuwa na mke mwingine."

Alipopewa fursa ya kuzungumza na Purity hewani alisema, 'Mimi nilikuwa nakupenda sana. Sijui nini ilitokea nyumbani hadi ukaenda. Naomba unifungulie simu tuambiane ukweli. Ikiwa ngumu ni sawa."