"Kama unamtaka mchukue!" Gidi azomewa vikali na jamaa hewani akijaribu kumpatanisha na mkewe

"Mimi nipelekeni hospitali. Hii kaziii wueh.. Jamaa ananiguezia bana, anasema niko na bibi yake," Gidi alilalamika.

Muhtasari

•Gidi alikabiliwa na wakati mgumu siku ya Jumatatu asubuhi wakati alipokuwa akijaribu kuwapatanisha wanandoa.

•Gidi alipojaribu kumuuliza ukweli wake kuhusu kilichotokea na kujua msimamo wake, Benjamin aligeuka kuwa mkali.

Image: RADIO JAMBO

Mtangazaji Gidi Ogidi alikabiliwa na wakati mgumu siku ya Jumatatu asubuhi wakati alipokuwa akijaribu kuwapatanisha wanandoa waliokuwa wamezozana baada ya miaka mitano ya ndoa.

Winfred Auma ,23, alikuwa ametuma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Benjamin Omondi ,34, ambaye alikosana naye  mwezi Juni mwaka huu na kutorokea kwao  huku akitumai angemfuata. 

Benjamin hata hivyo hajamfuata na kulingana na Winfred, hata hajawahi kujitambulisha rasmi kwa wazazi wake.

"Tulikaa naye karibu miaka 5. Tangu tuoane hajawahi kuonana na wazazi wangu. Wazazi wangu walianza kumwambia kwa nini amenioa na bado hawajazungumza. Aliambiwa aende akasema hawezi kuja saa hii. Alisema atafikiria alafu atakuja,"  Winfred alisimulia.

Aliongeza, "Tena alikuwa na madharau tu, alikuwa akinitishia maisha, ananichapa. Wazazi waliniambia niende anifuate. Mpaka sasa hajanifuata. Akiambiwa akuje anakataa anasema kama nataka kurudi nirudi lakini kama sitaki niache."

Winfred alisema alienda na mtoto mmoja ambaye aliolewa naye na mumewe akabaki na mtoto wao mdogo ambaye alizaa naye.

Benjamin alipopigiwa simu aliweka wazi kwamba Winfred ni mkewe na kubainisha kuwa hata wamekuwa wakizungumza.

"Mimi sikuenda shule. Sijui Kiswahili... Yeye ni bibi yangu. Hata juzi nimeongea na yeye," Benjamin alisema.

Gidi alipojaribu kumuuliza ukweli wake kuhusu kilichotokea na kujua msimamo wake, Benjamin aligeuka kuwa mkali.

"Kwani wewe ni baba yake ama ni baba yangu juu amekuletea kesi. Fanya hivi, wewe kwako kumekamilika kabisa? Kuna vitu unaingilia na hujui. Kamilisha kwako achana na mimi. Huyo ni bibi yangu achana na yeye. Wewe ni baba yangu ama yake? Kama unamtaka mchukue. Wacha kunisumbua," Benjamin alimfokea Gidi.

"Huyo ni bibi yangu, huwa naongea na yeye kila siku. Wachana na huyo mwanamke ni wangu. Wewe shughulika na maisha yako. Achana na mimi," alisema kabla ya kuanza kunena na watu ambao walikuwa naye.

Ilibidi Gidi akate simu hiyo kwani jamaa huyo alianza kutumia lugha ya matusi hewani, jambo ambalo halikubaliki.

"Mimi nipelekeni hospitali. Hii kaziii wueh.. Jamaa ananiguezia bana, anasema niko na bibi yake," Gidi alilalamika.

Winfred alisisitiza kwamba anampenda sana mumewe na kusema angependa sana kurudiana naye walee watoto pamoja. 

Hata hivyo, alisema kuna uwezekano jamaa huyo ana mahusiano mengine kwani aliwahi kumpata na msiachana barabarani.

Je, una maoni gani kuhusu Patanisho ya leo?