"Naweza hata kukukamata!" Jamaa azomewa vikali na mama mpenziwe kwa kumzuia amalize masomo

Mamake Hanet alimzomea Brian na kumlalamikia kwa madai ya kumharibia masomo binti yake.

Muhtasari

•Mamake Hanet alimbainisha Brian kuwa hataki kujihusisha na mahusiano yake na bintiye na kumtaka amruhusu amalize masomo.

•Brian alichukua fursa kumuomba msamaha mamake Hanet na kujaribu kumweleza kuhusu hali yake na binti yake.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Jamaa aliyejitambulisha kama Brian Wekesa ,20,  kutoka Kakamega alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mpenzi wake Hanet Hongo ,20, ambaye alitoroka mwezi uliopita.

Brian alisema mahusiano yake ya takriban mwaka mmoja yalianza kuyumba mwezi jana baada ya mpenziwe kusema ameenda nyumbani kumuona mama yake.

Alisema Hanet alienda akiwa na ujauzito wa mtoto wao wa kwanza.

"Tulikuwa tunakaa naye vizuri akasema ameenda kumuona mama yake kidogo. Sasa amekaa nyumbani hata amekataa kuwasiliana nami.Sijui kama nilikuwa nimekosea," Brian alimwambia mtangazaji Gidi.

"Awali tulikuwa tunaongea naye vizuri akasema ameenda kumuona mama yake juu ni mgonjwa. Kufika akaanza kusema mtu nilikuwa naongea naye sio yeye.

Nilikuwa nashughulikia mahitaji nyumbani. Sijaongea na mwanadada mwingine. Bado sijalipa mahari," alisema Brian.

Kwa kuwa Hanet hana simu kwa sasa, Brian alitoa namba ya mama yake ambaye alipatikana baada ya majaribio kadhaa.

Mamake Hanet aliposhika simu alitumia fursa hiyo kumzomea Brian na kumlalamikia kwa madai ya kumharibia masomo binti yake.

"Maneno yenu sijaelewa ni nini mbaya. Huwa haniambii vile mko. Siwezi kujua maneno yenu kabisa," Mamake Hanet alimwambia Brian.

Aliendelea, "Wewe Hanet anakuja kwako na sijui. Wewe ndiye umefanya hata course hajafanya. Wenye walikuwa wamemchukua wamemtafuta sana. Wenzake walifanya mtihani na yeye hakuweza kufanya. Nina uchungu na wewe sana. Unataka kuoa mtu na huna mbele wala nyuma na unamchukua kama hajamaliza course. Mimi nimelipa course, pesa imeenda bure. Ungemruhusu aje afanye mtihani." 

Mamake Hanet alimbainisha Brian kwamba hataki kabisa kujihusisha na mahusiano yake na bintiye na kumtaka amruhusu amalize masomo.

"Maneno yako na Annete siwezi kujua. Na sitaki kujua, Ati ni bibi yako, bibi yako kutoka lini? Wewe naweza ata kukukamata wewe. Mtoto wangu anafaa kusoma unasema unampeleka Radio Jambo eti ni bibi yako, ni mke wako kutoka lini?" Mamake Hanet alimwambia Brian.

Aliendelea kulalamika, "Hanet sasa amerudi nyuma. Mwezi wa nne atarudi kufanya kozi. Brian alikuwa amekataa kumpatia transport, ndugu yake ndiye alimtumia nauli. Wanajadiliana nini kwa radio, ametoa ng'ombe wangapi? Hanet alikuwa amepata watu wanamchukua bure, yeye ndiye nataka aendelee ati Brian anamchukua!"

Kwa kumalizia, mamake Hanet alimwambia Brian, "Sijakujua na sijakuona sijui unafanana aje. Patia Hanet nafasi amalize course yake. Na siku atakuja kwenu jua atapatikana. Mimi nataka tu amalize course. Maisha ya saa hii watu wanafaa kutafuta wote." 

Brian pia alichukua fursa kumuomba msamaha mamake Hanet na kujaribu kumweleza kuhusu hali yake na binti yake.