Patanisho: Jamaa amkataza mkewe kuajiriwa hotelini akihofia atatongozwa na mwanamume mwingine

Kelvin alieleza wasiwasi wake kuhusu mkewe kufanya kazi kwa hoteli akisema huenda akanyakuliwa na mwanaume mwingine.

Muhtasari

•Kelvin alisema ndoa yake ya miaka mitatu ilisambaratika baada ya mkewe kuondoka nyumbani mwezi Desemba na kutorejea tena.

•Charity alipinga hatua ya Kelvin kumzuia kufanya kazi kwa hoteli akisema alitaka afanye kazi ili asaidie familia yake.

Image: RADIO JAMBO

Kelvin Kipkemboi (27) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Charity Osore (23) ambaye alimuacha mwishoni mwa mwaka jana.

Kelvin alisema ndoa yake ya miaka mitatu ilisambaratika baada ya mkewe kuondoka nyumbani mwezi Desemba na kutorejea tena.

Pia alifichua kwamba alikuwa amempiga mke wake baada ya kuzozana kabla hajaondoka.

"Bibi yangu alitoka Desemba 24, lakini tulikuwa tumekosa Desemba 23. Tulikuwa tumegombana kidogo, nikampiga kidogo," Kelvin alisema.

Aliongeza, "Alitaka kuenda nyumbani nikamwambia sina pesa wakati huo asubiri. Nilimpiga lakini nikamuomba msamaha. Alisisitiza kwenda nyumba Desemba 24 arudi 31. 31st ilipofika nilimpigia simu akawa harudi."

Alikiri kwamba ilikuwa mara ya pili kumpiga mkewe wakati alipochukua hatua ya kuondoka.

"Nikimuuliza akuje anasema anakuja tu. Ilikuwa mara ya pili kumpiga. Ni hasira tu hutokezea lakini naomba msamaha," alisema.

Charity alipopigiwa simu aliweka wazi kwamba sio rahisi kwa yeye kurudiana na Kelvin.

"Saa hizi ni ngumu. Nimeishi na Kelvin lakini nikimwambia asaidie familia yangu hataki. Mamangu aliaga dunia mwezi wa nane, tulitaka kufanya makumbusho nikamwambia alete ng'ombe kwa kuwa hajawahi kunilipia mahari.Wazazi wake walisema haiwezekani. Mambo yake ni ngumu siwezi kurudi, "Charity alisema.

Alimwambia Kelvin, "Wewe hakuna kitu utanisaidia kwa maisha yangu. Unipatie wakati, kunichapa ulinikosea. Huwa unafanya hivyo kila wakati kunichapachapa kila wakati. Ulipata pesa na ulinituma kwetu bila hata sukari."

Charity alisema anajua mumewe hajafanikiwa sana kifedha ila anamuelewa.

Hata hivyo alipinga hatua ya Kelvin kumzuia kufanya kazi kwa hoteli akisema alitaka afanye kazi ili asaidie familia yake.

"Sitaki mambo yake anaweza kuniua wakati wowote. Amenichapa mara nne. Tena alitusi familia yangu. Kama anataka nirudi huko, akuje nyumbani kwanza. Hata alikosea mamangu mdogo.

Akisaidia familia yangu tutaelewana. Akiweka kiboko chini pia ni sawa. Nikimwambia niende kazi hataki. Anataka tu  nikae kwa nyumba," Charity alisema.

Kelvin alieleza wasiwasi wake kuhusu mkewe kufanya kazi kwa hoteli akisema huenda akanyakuliwa na mwanaume mwingine pale.

"Nilimwambia kazi ya hoteli .Kazi ya hoteli bibi yangu ataenda bana, atachukuliwa. Nilimwambia nitamuwekea biashara," alisema.

Aidha, alisema atajipanga hivi karibuni aende nyumbani kwa kina mkewe.

Kelvin alimwambia Charity, "Wewe ndiye mke wangu, sina mwingine. Nakupenda kama nyama choma.'

Charity alimwambia, "Funga safari ukuje kwetu maana nakupenda."