Patanisho: Mama ajuta kumtusi mwanawe wa miaka 19 kwa kuhama nyumbani, kutomlipia dadake karo

Bi Maggy alisema alimkasirikia sana mwanawe hadi kumtumia ujumbe mbaya ambao uliharibu uhusiano wao.

Muhtasari

•Bi Maggy alisema uhusiano wake na mwanawe uliharibika baada ya yeye kumtaka kijana huyo mwenye umri wa miaka 19 amlipie karo dadake mdogo.

•Sam alipopigiwa simu, mama yake alichukua fursa hiyo kumuomba msamaha ila akakata simu kabla hawajazungumza.

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, mwanamke aliyejitambulisha kama Maggy Lenduda (33) kutoka Samburu alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mwanawe Sam Lenduda ambaye alikosana naye mwishoni mwa mwaka jana.

Bi Maggy alisema uhusiano wake na mwanawe uliharibika Desemba mwaka jana baada ya yeye kumtaka kijana huyo mwenye umri wa miaka 19 amlipie karo dadake mdogo, jambo ambalo hangeweza kwani hakuwa na kazi.

Alisema alimkasirikia sana mwanawe hadi kumtumia ujumbe mbaya ambao uliharibu uhusiano wao.

"Kijana yangu alimaliza shule akasaka kibarua. Nikamwambia asisahau sisi tulio nyumbani, nikamwambia wakati akipata kibarua atukumbuke sisi nyumbani," Maggy alisimulia.

Aliongeza, "Alienda Nairobi na kukatiza mawasiliano. Kuna kijana alitoka Nairobi akaja nyumbani na akaniambia kijana wangu bado hajapata kazi, nikamtumia meseji mbaya. Nilimuuliza mbona alienda Nairobi na hakuna mawasiliano. Sikujua kwamba hakuwa amepata kazi."

Sam alipopigiwa simu, mama yake alichukua fursa hiyo kumuomba msamaha ila akakata simu kabla hawajazungumza.

Bi Maggy alisema, "Nikijaribu kumpigia anasema yuko bize. Wakati mwingine nikimpigia anakata simu. Mimi sina bwana, ni mtu najitegemea. Aliondoka tu hivyo akatuacha nyumbani.

Sikutusi yeye, nilimuuliza ameondoka akaanza kujishughulikia. Labda ameenda akapata boma na msichana akaanza kushughulikia yeye na kutusahau."

Alipopewa fursa ya kumuomba mwanawe msamaha hewani, Maggy alisema, "Mimi bado ni mama yake na hakuna mahali atapata mwingine. Akumbuke tu mahali tumetoka, ajaribu kukumbuka maisha ya nyumbani. Naomba awe huru kwangu na mimi niwe huru kwake ili tuweze kusaidiana maishani."

Je, maoni yako ni yepi kuhusu Patanisho ya leo?