Patanisho: Mke achoma nguo na kutoroka baada ya mumewe kumkataza kuzungumza na majirani

Wambua alikiri kwamba yeye na mkewe kwa kawaida huwa wanapigana nyumbani na kurudiana kama watu wazima.

Muhtasari

•Wambua alisema mkewe aligura ndoa yake ya miaka minne na kurudia kwao Disemba mwaka jana kufuatia mzozo wa kinyumbani.

•Wambua alieleza wasiwasi wake kuhusu kwenda nyumbani kwa kina mkewe huku akieleza kwamba wazazi wake wanaamini alimtishia binti yao.

Image: RADIO JAMBO

Peter Wambua ,31, kutoka kaunti ya Kiambu alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Matilda Kalunda ,31, ambaye alikosana naye mwisho mwa mwaka jana.

Wambua alisema mkewe aligura ndoa yake ya miaka minne na kurudia kwao Disemba mwaka jana kufuatia mzozo wa kinyumbani.

"Mke wangu nimekaa naye miaka nne karibu tano, nilimuoa na watoto wawili, tukazaa mmoja naye. Alikuwa amezoea kukaa kwa majirani nikienda kazi. Ni wanawake. Siku moja nilimpata kwa majirani usiku, sikumuuliza. Siku iliyofuata, nilimuuliza kwa nini anashinda kwa majirani akakasirika, akachukua nguo akawekelea kwa jiko ya makaa," Wambua alisimulia.

Aliongeza, "Alichukua nguo zilizokuwa kwenye begi akawekelea kwa jiko lakini nikatoa. Alipoona nimetoa aliona kama nitampiga akaenda. Alichukua mtoto wakaenda naye. Huwa tunaongea lakini anasema nimuendee kwao. Nilimpigia mamake akaniuliza namtafutia nini na nilisema nitamuua. Mimi sikusema hivyo. Niliuliza watu ambao ningeenda nao wakasema hakuna haja niende huko. Kama namtaka ajilete."

Wambua alieleza wasiwasi wake kuhusu kwenda nyumbani kwa kina mkewe huku akieleza kwamba wazazi wake wanaamini alimtishia binti yao.

"Mama mkwe na baba mkwe wanajua nilisema nitamuua. Naogopa. Nimejaribu kumshawishi lakini pia yeye anaogopa," alisema.

Juhudi za kumpata Bi Matilda ili kumpatanisha na mumewe hazikufua dafu. Hata hivyo, Gidi aliweza kumpata mamake Matilda ambaye alifunguka mengi kuhusu ndoa ya wawili hao.

"Msichana wangu aliniambia anateseka. Aliniachia hao watoto. Mimi nilikuwa nashughulika na wao, hakuna kitu alikuwa ananitumia. Hata simu hakuwa ananipigia. Kama mzazi nilikuwa na stress," mamake Matilda alifunguka.

Aliongeza, "Alitumia simu ya jirani akaniambia amefukuzwa kwa nyumba, na sio mara moja. Aliniambia amepigwa kichapo kibaya sana. Nimwambie aende wajadiliane aone kama atalala kwa hiyo nyumba. Akaniambia akirudi kwa hiyo nyumba atamuua. Mimi nilishughulika hadi akapata nauli ya kuja nyumbani. Akanieleza vile amekuwa akiteseka. Nikamwambia atulie hapo nyumbani tusaidiane. Ananiambia eti hata akirudi ni shida kwa sababu yeye ndiye anashughulikia kila kitu."

Wambua alijitetea kwa kusema, "Mimi nilikuwa nashughulika nyumbani. Hizo vitu alienda kusema nyumbani ni uongo. Aliniambia alisema kutokana na hasira. Hapo kwa nyumba huwa tunapigana  sisi wote. Huwa tunapigana sisi wote na tunarudiana kama watu wazima.. Hiyo kitu alikwambia ni uongo."

Mamake Matilda alimwambia, "Siwezi kuingilia mambo ya ndoa yenu. Kama mnarudiana ni sawa lakini chukua watoto wote mkae na wao."

Aliongeza, "Kama angependa mke. Mimi sijawahi kumuona, ata simjui na amekaa na msichana wangu hizo miaka yote. Kama anataka mke akuje nyumbani amuone. Huyo Mwendwa anasema hamjui."

Je, ushauri wako ni upi?