Jamaa akosana na mkewe baada ya kutoka kutazama Arsenal ikiiadhibu Sheffield 0-6

Lameck alisema ndoa yake ya mwaka mmoja imekuwa na misukasuko ambayo ilikithiri usiku wa Jumatatu.

Muhtasari

•Lameck alisema Bi Kerubo alikosa kuelewa kwamba alikuwa ametoka kutazama mpira na badala yake akamshtumu kwa kuenda nje ya ndoa.

•Lameck alieleza kwamba hata hivyo amekuwa akizozana na mkewe kwa muda mrefu.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Lameck Rioba Misiori ,35, kutoka Kisii alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Anne Kerubo ambaye alikosana naye usiku wa kuamkia Jumanne.

Lameck alisema ndoa yake ya mwaka mmoja imekuwa na misukasuko ambayo ilikithiri usiku wa Jumatatu wakati alipoenda kutazama mechi kati ya Arsenal na Sheffield United.

Alisema Bi Kerubo alikosa kuelewa kwamba alikuwa ametoka kutazama mpira na badala yake akamshtumu kwa kuenda nje ya ndoa.

"Nilienda kutazama game ya Arsenal. Nikirudi akasema nimetoka umalaya. Nikamwambia mimi sijatoka umalaya. Nikaona hatuelewani," Lameck alisema.

Aliongeza, "Nilimwambia mtu hununua mayai ukifika kwa mlango inapasuka. Alilala kufika asubuhi akasema nimesema nataka kumyonga. Ametoka ameenda kazi."

Lameck alieleza kwamba hata hivyo amekuwa akizozana na mkewe kwa muda mrefu.

"Amekuwa akinitishia. Kuna vile kutoka nyuma tumekuwa tukivurugana. Kutokana na maongezi yake, ni kama anataka kutoroka," alisema.

Bi Kerubo alipopigiwa simu, Lameck alitumia fursa hiyo kuomba msamaha na kumsihi mkewe atulize moyo wake.

"Nakuomba unisamahe. Mahali nilikuwa nimekukusea naomba unisamahe. Hiyo maneno eti nataka kukunyonga sikumaanisha hivyo, naomba unisamehe. Naomba utulie tuendelee na maisha yetu vizuri," alisema.

Bi Kerubo alisema, "Siwezi nikasamehe mtu anasema ataniua. Anasema anataka kuniua mara nyingi tukizozana. Ni mazoea. Nilimwambia nitaenda kwa polisi niandikishe taarifa na tuachane. Nimejaribu kuvumilia lakini nimechoka."

Alidai kwamba ni mazoea ya mumewe kuzozana naye kuhusu mambo madogo madogo na kutishia maisha yake.

"Alisema mtu anasema anazaa mtoto anakufa, unanunua mayai yanakufa. Hapo siwezi nikamnamehe," Bi Kerubo alisema.

Aliongeza, "Mimi nikipata pesa natoka nahama. Siwezi nikakaa na mtu anataka kuniua."

Wawili hao hawakuweza kupatana kwani Bi Kerubo alikata simu yake. Je ushauri wako ni upi?