Patanisho: Jamaa ajuta kutishia kumuua babake baada ya kunywa chang'aa, aapa kuacha chupa

"Nilisema akiendelea hivyo naweza nikamuua. Lakini sasa naomba msamaha.. Nilikuwa nimekunywa chang'aa," Emmanuel alisema.

Muhtasari

•Emmanuel alidokeza kuwa wamezozana na babake kuhusu ulevi wake na akadai kuwa alihisi mzazi huyo wake alikuwa akimbagua.

•Emmanuel alisema hakuna shida yoyote iliyompelekea kuomba msamaha na kuweka wazi kuwa alitaka tu kupatana na mzazi wake.

Image: RADIO JAMBO

Jamaa aliyejitambulisha kama Emmanuel Makokha ,24, kutoka kaunti ya Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na baba yake mzazi Robert Makokha Muchele ,60, ambaye alikosana naye mwaka jana.

Emmanuel alisema uhusiano wake na babake uliharibika mwezi Disemba mwaka jana wakati alipomuongelesha vibaya.

Aidha, alidokeza kuwa wamezozana na babake kuhusu ulevi wake na akadai kuwa alihisi mzazi huyo wake alikuwa akimbagua.

"Mwezi Disemba tulikosana na baba yangu kwa sababu ya pombe. Kuna vile aliongelesha vibaya mpaka mimi nikaamua kumjibu.

Nilisema akiendelea hivyo naweza nikamuua. Lakini sasa naomba msamaha.. Nilikuwa nimekunywa chang'aa,"  Emmanuel alisema.

Bw Robert alipopigiwa simu alikiri kwamba mwanawe alitishia kumuua ila akabainisha kuwa hakuchukulia hilo kwa uzito.

"Kweli, alikuwa anaongea hivyo. Mimi sikuchukulia kwa uzito," Bw Robert alisema.

Emmanuel alimwambia babake, "Acha nikuombe msamaha kwa yale niliongea kwa sababu nilikuwa nimechanganyikiwa kidogo. Naomba unisamehe sitarudia, juu wewe ni mzazi na sifai kuongea kama nilivyoongea."

Bw Robert alikubali ombi la msamaha la mwanawe ila akamshauri aache kutumia mihadarati.

"Mimi nimekubali msamaha lakini utaacha pombe na sigara?" alimuuliza mwanawe.

Emmanuel alimjibu, "Pombe nimeacha.Ndiyo, saa hii situmii kitu. Ata ilifanya nitoke nyumbani kwa sababu nilikuwa na marafiki ambao walikuwa wanafanya niende vibaya. Saa hii niko Nairobi nafanya kazi."

Bw Robert alisema, "Kama pombe ndio inafanya ukose na umeacha nakubali msamaha.. Nimemsamehe kabisa. Wakati alikuwa anakunywa alikuwa anakosea anasema ataniua."

Emmanuel alisema hakuna shida yoyote iliyompelekea kuomba msamaha na kuweka wazi kuwa alitaka tu kupatana na mzazi wake.

"Mimi sina shida. Yeye ni mzazi wangu lazima nimuombe msamaha. Mimi niko sawa hapa Nairobi. Nilikuwa nikikunywa kwa sababu nilikuwa na marafiki zangu," Emmanuel alisema.

Aliongeza, "Baba naomba unisamehe. Nairobi nilikuja juu ya kazi naishi vizuri. Kwa yale niliongea naomba."

Bw Robert alisema, "Nimefurahi vile ameacha chang'aa. Nimefurahi kuskia sauti yake kwa simu. Nimekubali msamaha."