Patanisho: Jamaa amsamehe mpenziwe licha ya kutangatanga, kuolewa kwa miezi 6 baada ya kutengana naye

Christine alikiri mumewe alikuwa akimpata akitaniana na wanaume wengine kwenye mtandao wa Facebook.

Muhtasari

•Christine alikiri kuolewa na mwanaume mwingine kwa takriban mwaka nusu baada ya kutengana na Bw Anthony Ruthari.

•Bw Anthony alipopigiwa simu alilalamika kwamba mpenziwe huyo alikuwa amezoea kufanya mambo ya kumfanya akasirike.

Ghost na Gidi studioni
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, mwanadada aliyejitambulisha kama Christine Muthoni ,22, kutoka Nyeri alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Antony Ruthari ,34, ambaye alitenagana naye mwaka jana.

Christine alisema ndoa yake ya mwaka mmoja ilivunjika Juni mwaka jana baada ya mumewe kupata akitaniana na wanaume wengine kwenye mtandao wa Facebook.

Aidha, alikiri kuolewa na mwanaume mwingine kwa takriban mwaka nusu baada ya kutengana na Bw Ruthari.

"Ilikuwa tu makosa kidogo ya nyumba tu. Alikuwa ananipata tu na mambo ya ukora ukora. Ilikuwa tu mambo ya Facebook. Alikuwa akaona vile huwa tunaandikiana meseji huko na wanaume wengine. Tena nikatoka nikaenda kwa mwanaume mwingine nikaolewa miezi sita, ni kama ilikuwa come we stay. Nilikuwa natafuta tu mahali ya kukaa, nikaenda nikaolewa. Nilikaa miezi sita, nikiwa kwa jamaa huyo nilikuwa bado naongea na yeye," Christine alisimulia.

Aliongeza, "Nilitaka tu kuomba msamaha na kumwambia aache kunishuku. Tulikosana na huyo jamaa mwingine, anajua. Alikuwa anajua nina wanaume wengi lakini niliachana nao .Nataka kuomba msamaha na kumuomba nirudi, na aache kunishuku. Alikuwa anamuona huyo jamaa kwenye Facebook. Alikuwa anaona watu wananiita baby baby na hajui ni kina nani. Kabla nipatane na yeye nilikuwa nimepatana na mwingine tukaenda Nairobi. Nilikuwa nataka unisamehe yote na uache kunishuku shuku."

Bw Anthony alipopigiwa simu alilalamika kwamba mpenziwe huyo alikuwa amezoea kufanya mambo ya kumfanya akasirike.

"Huwa unasema hivyo leo, alafu kesho unanikasirisha tena. Umezoea. Kama uko sure hutarudia tena ani sawa. Lakini kama kila wakati ni mambo ya uongo haitawezekana," Anthony alisema.

Christine alimwambia, "Sitafanya hivyo tena., Nataka tukae vile tulikuwa tunakaa vizuri kitambo. Wewe huna makosa.Sijui ni nini ilikuwa imenishika aki ya Mungu. Mimi ata niliombewa, hiyo mambo iliisha."

Anthony alifichua kwamba alikuwa amekaa na Christine kwa muda mfupi na akaweka wazi kwamba alikuwa amemkubali pamoja na mtoto.

Gidi alimshauri Christine kutulia na kuacha kurukaruka kisha akamlazimisha kula kiapo cha kutotangatanga nje.

"Mimi Christine Muthoni nimeapa ya kwamba nimeacha kutangatanga. Nataka kukaa na Antony kama bwanangu. Sitatoka tena kutangatanga. Ewe Mungu nisaidie," Christine aliapa.

"Nakuwanga nimekupenda sana. Sitaenda kwa mwingine," alimwambia mumewe.

Anthony alisema, "Nampenda sana, ndio maana akienda na huko huwa namfikia. Mimi nitampea hiyo chance."

Je, una ushauri ama maoni gani kuhusu Patanisho ya leo?