Patanisho: “Mume wangu ana hulka ya kutoka nje ya ndoa lakini bado nampenda, nisaidie turudiane!”

“Mimi nampenda lakini chenye anafanya ndicho kinanipandisha hasira, sina nia ya kutangatanga nje sasa hivi dunia ni mbaya maisha ni magumu….” Mrembo huyo aliomba.

Muhtasari

• Kepha alisisitiza kwamba mkewe huwa anamshuku kila mara tu anapokosa kushika simu yake au kujibu ujumbe wake, akimtaka kubadili mawazo yake kumhusu.

GIDI NA GHOST
GIDI NA GHOST
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho kwenye Gidi na Ghost Asubuhi ndani ya stesheni yako pendwa ya Radio Jambo, mrembo kwa jina Esther mwenye umri wa miaka 26 kutoka Oyugis kaunti ya Homabay alitaka kupatanishwa na mume wake kwa jina Kepha Oduor mwenye umri wa miaka 35.

Esther alisema kuwa wamekaa kwa ndoa kipindi cha miaka 5 na wana watoto 2, mmoja akiwa ni yule aliyeingia naye kwenye ndoa hiyo.

Alisema kwamba walikosana na mume wake wiki jana kutokana na msururu wa ugomvi kutokana na kile alichokitaja kuwa ni hasira zake baada ya kugundua mume wake anamsaliti kimapenzi.

Baada ya kukosana, mume wake aliamua kubaki Awasi anakofanya kazi huku yeye akisalia nyumbani kwao Oyugis.

Esther hata hivyo alisisitiza kwamba yeye bado anampenda mume wake licha ya kugundua anamsaliti kimapenzi mara kwa mara, akisema kuwa ni wivu na hasira zake zinazomsababisha kufanya vitu ambavyo havieleweki.

“Shida za ndoa yetu ni udanganyifu wa ndoa hii maneno ya kutoka nje, mimi mwenyewe ni mtu wa hasira sana ambayo hunifanya nifanye vitu vibaya, sana sana wakati anatoka nje ya ndoa na nijue, hiyo hasira ikishapanda huwa sisikilizi mtu,” Esther alisema.

Esther alisema kuwa huwa anamketisha mumewe chini na kuzungumza na mumewe huwa anamtuhumu kwamba ni kutokana na hasira zake ndizo zinamfanya kuenda nje ya ndoa.

“Huwa namuongelesha ananisikiliza lakini baadae anasema mimi ndio namsababisha kuenda nje ya ndoa kutokana na hasira zangu… huwa inaniumiza sana roho, huwa sijielewi juu ya hiyo wivu,” aliongeza.

“Mimi nampenda lakini chenye anafanya ndicho kinanipandisha hasira, sina nia ya kutangatanga nje sasa hivi dunia ni mbaya maisha ni magumu….”

Mumewe alipopigiwa simu, alimuuliza mkewe mbona kwanza aliamua kumpeleka kwenye Patanisho na mkewe akajitetea kwamba alifanya hivyo kwa sababu anampenda na alitaka dunia nzima isikie kuwa anampenda na anataka warudiane.

Alisema kwamba alitoka na hasira na ndio maana aliamua kunyamaza kisa hataki mambo mengi akisema, “Chenye kinaleta shinda ni hiyo mambo ya simu, nimeenda kazi halafu unitumie ujumbe nikose kujibu huwa unakasirika, na nilikuambia siwezi kuacha kuhudumia mteja na nichukue simu yako tuongee na huyu mteja nimemuacha pembeni.”

Kepha alisisitiza kwamba mkewe huwa anamshuku kila mara tu anapokosa kushika simu yake au kujibu ujumbe wake, akimtaka kubadili mawazo yake kumhusu.