•Morris alisema uhusiano wake na babake uliharibika mwaka wa 2022 wakati alipomtusi baada ya kumuomba pesa akakataa.
•Bw Elijah alipopigiwa simu, alikana kumjua Morris na kubainisha kwamba hana mtoto yeyote nje.
Kijana aliyejitambulisha kama Morris Muchira ,18,kutoka Murang'a alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na baba yake mzazi Elijah Mutethi ,42, ambaye alikosana naye takriban miaka miwili iliyopita.
Morris alisema uhusiano wake na babake uliharibika mwaka wa 2022 wakati alipomtusi baada ya kumuomba pesa akakataa.
Pia alieleza jinsi babake alikataa kumpa ruhusa wakati alipoomba kwenda kutahiriwa.
"Tulikuwa tunachat na yeye ikafika mahali nikamtumia matusi. Nilikuwa na miaka 16. Ni ile tu nilikasirika nikamtusi. Baada ya kumaliza shule, nilienda kumomba ruhusa ya kutahiri akakataa. Nikaenda kwa uncles zangu wakakubali," Morris alieleza.
Pia alidai kwamba mzazi huyo wake alikataa kumpa kitambulisho chake wakati alipotaka kuandikisha chake.
Bw Elijah alipopigiwa simu, alikana kumjua Morris na kubainisha kwamba hana mtoto yeyote nje.
"Sikumbuki hayo, na simjui. Watoto wangu niko nao nyumbani, sina mtoto nje," alisema Elijah.
Morris alisema, "Ako na watoto wawili wengine ambao alizaa na mamangu. Mimi ni mzaliwa wa tatu. Nilitoka huko nikiwa mdogo. Huwa anasema mimi ni wa mama. Hadi birth certificate ni jina lake. Hadi cheti cha KCSE ni jina lake. Wakati nilimuomba kitambulisho nikachukue changu anasema hajui mahali aliweka. Nikimuomba birth certificate anasema hajui mahali aliweka."
Morris alisisitiza kwamba Bw Elijah ni mzazi wake.
"Sijawahi kuskia akisema mimi sio mtoto wake,' alisema.
Je, una maoni ama ushauri gani kuhusu Patanisho ya leo?