•Marwa alisema ndoa yake ya mwaka moja ilisambaratika Mei wakati mkewe alipotoroka ghafla bila kumpa sababu.
•Mtangazaji Gidi hata hivyo alichukua fursa kumshauri kijana huyo na kumueleza waziwazi utata uliozingira ndoa yake.
Paul Marwa ,23, kutoka Migori alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Sarah Boke ,20, ambaye alikosana naye mapema mwaka huu.
Marwa alisema ndoa yake ya mwaka moja ilisambaratika Mei mwaka huu wakati mkewe alipotoroka ghafla bila kumpa sababu.
"Alitoka nyumbani tu, sikujua shida ni nini. Nilitoka kazi nikamkosa, sikujua shida ilitokea wapi, na sikuwa nimemkosea. Nilikuwa nimemchagua awe mke wangu na tuishi milele," Marwa alisema.
Alisema licha ya kuwa anawajua wakwe zake, hajakuwa akiwasiliana nao. Hata hivyo, aliomba kusaidiwa kujua msimamo wa mkewe.
Juhudi za kumpatanisha Marwa na mpenziwe hata hivyo hazikufua dafu kwani Bi Sarah hakushika simu yake.
Mtangazaji Gidi hata hivyo alichukua fursa kumshauri kijana huyo na kumueleza waziwazi utata uliozingira ndoa yake.
"Hukuwa umemuoa rasmi. Mlikuwa tu marafiki. Ni mwanadada ambaye ulikuwa unaishi naye tu na hujui mipango yake. Ndio maana aliondoka kama mwizi.. Unakuja Nairobi unaacha msichana mdogo wa miaka 20 nyumbani. Huoni hapo ulifanya makosa?" Gidi alimwambia Marwa.
Marwa alikiri kwamba ni kweli alikosea kumuacha mkewe nyumbani. Hata hivyo, alibainisha kuwa mpenziwe aliacha nguo zake nyumbani.
"Simu nikipiga anaweza shika, lakini kurudi ni kama bado anafikiria kama atarudi ama. Aliniambia ako Nairobi, nikamuuliza ama niende nimsalimie. Akasema haiwezekani kwa sababu yeye ni mgeni pale," alisema.
Alipopewa fursa ya kuzungumza na mpenziwe hewani, Marwa alisema, 'Mimi bado nakupenda. Ningependa urudi nyumbani tuishi pamoja kama zamani.."