•Latifah alisema babake ndiye amemlea tangu alipotengana na mama mzazi wake takriban miaka kumi na minne iliyopita.
•Alikiri kwamba mwanaume wa ukoo wao alimpachika mimba takriban miezi miwili iliyopita baada ya kumdanganya.
Mwanadada aliyejitambulishe kama Latifah Akumu mwenye umri wa miaka 17 kutoka Kakamega alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na baba mzazi wake Saidi Abdalla ,40, ambaye alikosana naye mapema mwaka huu.
Latifah alisema babake ndiye amemlea tangu alipotengana na mama mzazi wake takriban miaka kumi na minne iliyopita.
Alisema uhusiano wake na mzazi huyo mwenzake ulianza kusambaratika mapema mwaka huu wakati alianza kuzungumza na mamake.
"Baba na mama walitengana 2008, mama akaenda njia zake. Alienda Uarabuni miaka minne iliyopita. Huwa tunazungumza, hiyo kuongea ndiyo ilileta shida na babangu. Hakutaka tuzungumze. Nilimjua mama mwaka wa 2021, tangu atengane na baba sikuwa namjua.
Nilikuwa nataka kujiandikisha kwa mtihani na nilihitaji kitambulisho cha mama. Hapo ndio tukatafuta mama mzazi. Awali nilikuwa nikitumia kitambulisho cha mama wa kambo. Mama mzazi hakufurahi kwa nini watoto wake wanatumia kitambulisho cha mtu mwingine ilhali yeye yu hai," Latifah alisimulia.
Aliongeza, "Hatukuwa tunakaa vizuri na mama wa kambo. Baadaye nikaja nyumbani kwa kina baba Kakamega. Baba akapunguza usaidizi. Nyanya alijaribu sana mpaka akanirejesha shule. Kumbe kwa kina mama ni karibu, watu wa kina mama wakasema nitembee huko. Baba hakupenda vile nilienda huko, akanikujia."
Alikiri kwamba mwanaume wa ukoo wao alimpachika mimba takriban miezi miwili iliyopita baada ya kumdanganya.
"Baada ya usaidizi kupotea, na malumbano kwa familia, nilipata mimba. Niko na mimba ya miezi miwili. Bado tuko pamoja na mwanaume aliyenipachika mimba. Alikuwa amenidanganya ni mtu wa mbali, kumbe ni mtu wenye tuna mahusiano ya ukoo. Mambo yote baba anajua," alisema.
Bw Abdalla alipopigiwa simu, Latiffah alichukua fursa hiyo kumuomba msamaha.
Hata hivyo, Bw Abdalla alisikika kusitasita akibainisha kuwa bintiye alimuaibisha sana.
"Wewe si ulikataa kusoma. Nilikupeleka kwa nyanyako nikupeleke shule ukakataa. Ulijiona umefika, mbona unanitafuta sasa hivi na nilikuambia usinitafute. Mpaka walimu wanajua uko shule na huendi. Wewe unajua vile mimi nimekulea kwa shida. Kwa nini inafika mahali wewe unaniaibisha," Bw Abdalla alisema.
Kuhusu ujauzito wa bintiye, Bw Abdalla alisema, "Sasa imefika mahali umepachikwa mimba, hiyo mimba tutalelea wapi. Mimi sitaki stori za huyo kijana. Kama anataka kukuoa akuoe, mimi sitaki chochote kwenu. Huwa nahesabu ni kama sina mtoto. Uliniaibisha. Ata hujafika 18 years ushapata mimba!!"
Latiffah alijaribu kujitetea akisema, "Mama alisema nikae kwao. Alisema atanipeleka shule. Najua nilikosa ndio maana nakuomba msamaha. Niliacha shule nikiwa kidato cha pili. Ilikuwa 2023. Ilikuwa kukosa karo."
Bw Abdalla aliendelea kulalamika, "Huyo msichana nilikuwa naishi na yeye Mombasa. Mamake nilitengana naye akiwa na miaka miwili unusu. Alitoroka akaenda nyumbani eti kwa sababu shule aliitwa hakutaka, na hakutaka. Nilimwambie atafute shule huko Western. Nilienda nyumbani kumueleza mambo ya shule akanikimbia."
"Msamaha sijakataa lakini kuna shida. Hiyo mimba ni ya mjomba wake haswa. Huyo mjomba ameoa kwa boma yetu tena. Bibi ya huyo mjomba, anamuita auntie. Huyo auntie alimlea akiwa mdogo. Mahusiano iliharibika katika boma. Nilichoka. Hiyo kitu iliniuma sana.. Kumsamehea nimemsamehea lakini ajifikirie sana. Akiambiwa kitu na mzazi anasikia. Nilimwambia, chenye unatafuta utapata. Kitu yenye hana ni heshima," aliongeza.
Latiffah alimwambia babake, "Anisamehe. Najua amepitia magumu na mimi. Mbele nyuma nikiangalia naona hakuna mtu mwingine atanisaidia ila yeye. Binadamu hukosa. Nimekubali makosa yangu. Sikufanya kwa kujua. Anisamehe turejeshe uhusiano."
Bw Abdalla alimalizia kwa kusema, "Nimemsamehea lakini ajirekebishe, nitampigia simu tuzungumze."
Je, ushauri ama maoni yako kuhusu Patanisho ya leo ni yepi?