Patanisho: Jamaa ataka ex wake arudi awe mke mwenza, adai mkewe amekubali kukaa naye

"Bibi yangu alikuwa amekubali kukaa na yeye. Nataka huyu mwingine arudi awe mke mwenza," Richard alisema.

Muhtasari

•Richard alisema ndoa yake ya chini ya mwaka mmoja ilisambaratika Novemba mwaka jana wakati Judith alifunga virago kutoroka.

"Nilikuwa na bibi mwingine na alikuwa anataka kurudi, huyo kuskia hivyo akaenda. Huyu bibi mwingine amerudi," Richard alisema.

Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Jamaa ambaye alijitambulisha kama Richard Adera ,38, kutoka Siaya alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Judith Awino ,24, ambaye alikosana naye mwaka jana.

Richard alisema ndoa yake ya chini ya mwaka mmoja ilisambaratika Novemba mwaka jana wakati Judith alifunga virago kutoroka.

"Kuna pesa alikuwa anataka nikampatia. Nilienda kazi, kurudi nikapata kama amepanga virago vyake kama kwamba anapanga kuenda. Mimi nilienda safari ya kazi siku kumi. Nikiwa huko nilikuwa nampigia simu  anakata. Kurudi nilipata ameenda. Baadaye aliniambia ameenda na hataki mambo yangu," Richard alisema.

Richard pia alifichua kwamba mke wake wa zamani ambaye alikuwa ametengana naye alitaka kurudi na suala hilo pia lilichangia Judith kutoroka.

"Tulikuwa tumeagana yeye ni mke wangu. Nilikuwa na bibi mwingine na alikuwa anataka kurudi, huyo kuskia hivyo akaenda. Huyu bibi mwingine amerudi. Bibi yangu alikuwa amekubali kukaa na yeye. Tulikuwa tumekosana kwa sababu alitaka kuenda kazi mbali nikamkataza. Nataka huyu mwingine arudi awe mke mwenza," alisema.

Juhudi za kumpatanisha Richard na mpenziwe hata hivyo hazikufua dafu kwani Judith alikata simu punde baada ya Gidi kujitambulisha.

Gidi aliibua mashaka kuhusu Richard, ambayo jamaa huyo alitupilia mbali.

"You're lying. Vile nimekwambia ni ukweli. Mke wangu amekubali huyo msichana arudi," alisema.

Je, una maoni ama ushauri gani kuhusu Patanisho ya leo?