Patanisho: "Simpendi, niko na bwana! Ako na pesa ya kuharibu! Nikikosa pesa ya lunch nitamuitisha na atatuma!"- Mwanadada afoka

"Huyo jamaa ni mjinga. Simpendi, mimi niko na bwana. Alikuwa tu rafiki yangu," Millicent alisema.

Muhtasari

•Kelvin alisema ndoa yake ya chini ya mwaka mmoja ilisambaratika mwezi uliopita wakati mchumba wake aliondoka ghafla.

•Alipigiwa simu kwa mara ya pili ambapo alifunguka ukweli kwamba ameolewa na alikuwa akimtumia Kelvin vibaya tu.

Jamaa aliyejitambulisha kama Kelvin Khimisi ,26, kutoka Kariobangi alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mchumba wake Millicent Adhiambo ,25, ambaye alikosana naye hivi majuzi.

Kelvin alisema ndoa yake ya chini ya mwaka mmoja ilisambaratika mwezi uliopita wakati mchumba wake aliondoka ghafla.

Alidai kwamba alikaa na Millicent vizuri kwa miezi tatu kabla ya misukasuko kuingilia mahusiano yao.

"Mambo yangu na yeye haiendi vizuri. Kuna siku nilienda kazi, kurudi nikapata ameenda. Anasema mimi namtangaza kwa watu huko nje. Jana nilimuona nikamsimamisha kwa barabara akaniambia mtu wa kukaa na yeye kwa nyumba," Kelvin alisema.

Kelvin alikiri kwamba mpenziwe aliwahi kupata picha za wanadada wengine pamoja na jumbe za kutiliwa shaka za mpesa kwenye simu yake.

"Tulikaa miezi tatu vizuri. Hiyo ingine ilikuwa kusumbuana tu. Sikuwa nimemkosea. Ilikuwa tu mambo kidogo kidogo. Kuna vile alichukua akapata kuna picha za wanadada wengine. Pia akaenda mpesa akaona meseji kwamba natumia wanadada wengine pesa. Akasema namwambia sina pesa lakini natumia wanadada pesa. Kuna mwanadada nilikuwa naye kabla yake alikuwa anaitwa Maureen, alipata naongea naye na kumtumia pesa. Nilimwambia sina pesa lakini akaona natumia warembo pesa," alisema.

Millicent alipopigiwa simu kwa mara ya kwanza alisema, "Huyo mtu ni mjinga, aachane na mimi' kisha akakata simu.

Alipigiwa simu kwa mara ya pili ambapo alifunguka ukweli kwamba ameolewa na alikuwa akimtumia Kelvin vibaya tu.

"Huyo jamaa ni mjinga. Simpendi, mimi niko na bwana. Alikuwa tu rafiki yangu. Obweno ndiye bwanangu. Ni ujinga ako nayo. Huyo mtu ni mtoto, sitaki kuongea na yeye," Millicent alisema.

Kelvin alihoji, "Hiyo miezi tatu nilikuwa na yeye, huyo bwana yake alikuwa wapi? Alikuja nikampatia pesa ya njugu. Mimi sio mtoto na mimi sio mjinga, yeye ndiye amesema."

Millicent aliendelea, "Simpendi. Ako na pesa ya kuharibu. Mtu akikuita uende uchukue pesa, unaacha? Hana kazi ya pesa. Huyo mtu ni mjinga. Hakuwa analipa rent. Alitoa tu thao, thao inaweza lipa nyumba? Sasa mia nne ni ya njugu ama ni ya credit? Unaweza kaa na mtu anaropoka kila mahali? Simpendi."

Kelvin hata hivyo alitupilia mbali madai ya kusambaza maneno ya ndoa yake nje. Aidha, alidai kwamba Millicent hudai hampendi kisha baadaye anamtafuta.

"Huyo mtu siwezi mtafuta. Ata siwezi piga simu yake. Sina namba yake, nilimblock. Ata saai nikikosa pesa ya lunch nitamuitisha na atatuma," Millicent alisema.

Kelvin alimwambia, "Yeye akae maisha mazuri, tukipatana kwa barabara anisalimie. ata akiniona na mtu asilete fujo."

Je, una ushauri ama maoni gani kuhusu Patanisho ya leo?