Patanisho: Jamaa am'block mpenziwe miezi 3 kabla ya harusi baada ya kukataa ashike simu yake

"Alisema nimpatie simu.Nikamwambia hakuna kitu nimeficha lakini simpatii. Akakasirika akasema kuna kitu nimeficha," Nellie alisema.

Muhtasari

•Nellie alisema uhusiano wake wa mwaka mmoja ulivunjika wiki jana wakati alipokataa kumpa mpenziwe simu yake achunguze.

•Nellie alipoulizwa kama kuna kitu kingine alimfanyia mpenziwe, alisema, "Hakuna, ilikuwa tu hilo suala la simu."

Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Mwanadada mmoja ambaye alijitambulisha kama Nellie Nailantoi ,26, kutoka Nakuru alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mchumba wake Lameck Lusaba ,25, ambaye alikosana naye hivi majuzi.

Nellie alisema uhusiano wake wa mwaka mmoja ulivunjika wiki jana wakati alipokataa kumpa mpenziwe simu yake achunguze.

Alisema mpenziwe alim'block na hajazungumza naye tangu wiki iliyopita.

"Tulikuwa tumekaa, akasema nimpatie simu.Nikamwambia hakuna kitu nimeficha lakini simpatii. Akakasirika akasema kuna kitu nimeficha," Nellie alisema.

Alipoulizwa sababu ya kukataa kumpa mpenziwe simu yake, alisema, "Nilikuwa nimetoa jina lake kwa simu simu yangu, nikajua ingeleta shida. Hakuna mtu mwingine. Haongei na mimi, ameniblock kutoka wiki jana. Amekasirika kabisa. Ilikuwa mahusiano lakini tulikuwa tunapanga kufanya harusi Desemba. Nimejaribu kuongea na dada yake lakini bado haijazaa matunda. Alisema ananipea muda nijue nataka nini."

Juhudi za kumpatanisha Nellie na mpenziwe hata hivyo hazikufua dafu kwani Lameck alikata simu punde baada ya Gidi kumweleza sababu ya kumtafuta.

Nellie alipoulizwa kama kuna kitu kingine alimfanyia mpenziwe, alisema, "Hakuna, ilikuwa tu hilo suala la simu."

Je, ushauri ama maoni yako kuhusu Patanisho ya leo ni yepi?