Mwanadada alipiza kisasi kwa mumewe baada ya kumsikia akialika mpango wa kando alipokuwa anaugua

Muhtasari

•Irene alikiri kuwa aliamua kuwa na mahusiano na jamaa mwingine kama dhamira ya kulipiza kisasi kwa vile mumewe pia aliwahi kukanyanga nje ya ndoa hapo awali.

•Irene alifichua kwamba kando na mkewe kuwa na mahusiano mengine nje ya ndoa, pia aliharibu injini ya pikipiki kwa kuitia chumvi.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho mwanadada aliyejitambulisha kama Irene Imali (26) kutoka Kakamega alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mumewe Stephen (28).

Irene alifichua kwamba aligura ndoa yake mwezi jana baada ya mumewe kuchukua simu yake na kupata jumbe alizokuwa anatumiana na mwanaume mwingine.

Alieleza kuwa mumewe alimpiga vibaya baada ya kupata jumbe zile ambazo alikiri zilikuwa za mpango wake wa kando hadi akalazimika kutoroka.

"Mume wangu alipata jumbe za mpango wa kando kwa simu yangu. Baada ya kuzipata aliniuliza nikakataa kujibu kisha akanipigia ndipo nikakasirika nikaamua kuenda. Tumekuwa tukiongea lakini hatuelewani" Irene alisema.

Irene alikiri kuwa aliamua kuwa na mahusiano na jamaa mwingine kama dhamira ya kulipiza kisasi kwa vile mumewe pia aliwahi kukanyanga nje ya ndoa hapo awali.

"Hata kuna siku nilikuwa mgonjwa akaenda kuniongelea nyuma ya nyumba  eti 'hako ni kagonjwa kamelala'. Nilikuwa namskia tu akiongea. Nilichukua namba ya huyo msichana ili niongee naye. Kumuuliza aliniambia kwamba ako Webuye na eti bwanangu alimwambia kuwa mkewe alimuacha na kumwachia mtoto msichana. Hiyo ndiyo ilinikasirisha" Alisema.

Hali kadhalika Irene aliomba mumewe ashauriwe ahame kutoka eneo walilokuwa wanaishi huku akieleza kuwa hangependa kurejea mahali ambapo tukio lilitokea kutokana na aibu.

Stephen alipopigiwa simu alieleza kuwa tayari alikuwa ameomba mkewe waandae kikao na wazazi wao ili kusuluhisha mzozo wao.

Alifichua kwamba kando na mkewe kuwa na mahusiano mengine nje ya ndoa, pia aliharibu injini ya pikipiki kwa kuitia chumvi.

"Kitu kilichonikasirisha kabisa, alichukua chumvi akaweka kwa injini ya pikipiki. Ilinikasirisha kabisa moaka nikaona lazima maneno haya yakaliwe chini. Injini iliharibika ikabidi tena nitafute pesa niende gereji ndio itengezwe. Nilikuwa nimemwambia tukae chini tuongee kuhusu jumbe nilizopata. Nilipotoka nje kidogo nilipata amechukua funguo akafungua pikipiki akamwaga chumvi ndani" Stephen alisema.

Wawili hao  walikubali makosa yao, wakaombana msamaha na kuhakikishia kuhusu mapenzi yao.

Stephen hata hivyo alitupilia mbali suala la kuhama huku akieleza kwamba tayari alikuwa amehama mara nyingi hapo awali hadi kubandikwa jina 'mtu wa kuhamahama' na marafiki wake.