"Ni yeye ameoleka!" Jamaa aleta kesi akitaka kuoa wawili, mkewe afichua amewekwa na 'jimama' mjini

Dorice alifichua kwamba mwanamke ambaye mumewe anachumbiana naye amemzidi kwa umri na hata anaishi kwake.

Muhtasari

•Vincent alipoulizwa kuhusu mpango wake na Dorice, alidai kwamba yuko tayari kuwa na wake wawili kwani anatarajia mtoto na mke wa pili.

•Dorice alifichua kuwa alipogura ndoa yake, Vincent alioa mwanadada mwingine ambaye alitoroka kwa sababu ya mwanamke anayeishi na mumewe.

 

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Vincent Juma ,36, kutoka kaunti ya Kakamega alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Dorice Juma ,26, ambaye alikosana naye mapema mwaka jana.

Vincent alisema ndoa yake ya zaidi ya miaka kumi ilisambaratika wakati mkewe alipotoroka baada ya kuzozana na mama mkwe.

Aidha, alikiri kwamba alioa mke wa pili, jambo ambalo mkewe hakukubaliana nalo.

"Yeye alikorofishana na mamangu na akaondoka. Mimi sikukosana na yeye. Nilienda mpaka kwao, tukaongea na wazazi wake. Lakini alikuwa na dada yake ambaye alimpeleka Nairobi," Vincent alisimulia.

Aliongeza, "Unajua wakati mwingine huwa naenda kazi za nje. Wakati alipojua niko na mwanamke mwingine huko nje, akasema hawezi kukaa na mtu ako na mwanamke mwingine. Wakati alisikia niko na mke mwingine huku mjini, aliniachia watoto na akatoroka. Mpango wa kando haikuwa shida sana. Wakati walipokorofishana kidogo na mamangu ndio akatoroka. Bado niko na yeye huyu mwingine mjini."

Vincent alidai kwamba mkewe anafahamiana vyema na mwanamke ambaye anaishi naye mjini na hata huwa wanazungumza.

Alipoulizwa kuhusu mpango wake na Dorice, alidai kwamba yuko tayari kuwa na wake wawili kwani anatarajia mtoto na mke wa pili.

"Ni sawa niwe na wawili. Nataka wawili kwa sababu hata baba yabngu ako na watoto. Yeye (Dorice)  hakukubaliana na hayo maneno. Nataka huyo (Dorice) abaki kwa sababu niko na watoto na yeye ambao niko nao sasa hivi. Huyo mwingine huwa anakaa na mtoto mdogo, huyo mtoto mwingine huwa anakaa na mama yangu. Mimi ni mtoto kijana wa pekee. Tulipata naye watoto wawili wasichana. Huyu mwingine tuko karibu kupata mtoto naye. Tumekaa na Dorris miaka kumi," alisema.

Dorice alipopigiwa simu aliweka wazi kwamba hawezi akarudi kwa ndoa yake.

"Kurudi siwezi nikakubali juu mambo nilipitia ni mengi sana. Amesema kweli, Nikitoka alikuwa na mama, hiyo mambo ikaleta shida. Mimi niliamua niende nikae nyumbani na yeye abaki akitafuta. Kumbe alikuwa na mipango mingine ya kuwa na huyo mama. Ilileta shida mama mkwe pia naye akaingilia," Dorice alilalamika

Alidai kwamba mwanamke ambaye mumewe anachumbiana naye amemzidi kwa umri na hata anaishi kwake.

"Ni mama. Ni yeye (Vincent) ameoleka juu ni yeye anaishi kwake. Huyo Vincent anaishi kwa huyo mama. Mimi nikatupwa nyumbani na watoto, hanisaidii," Dorice alisema.

Aliongeza, "Mimi nimeshamove on, yeye aendelee na maisha yake. Saa hii lazima nijipee muda nitafute pesa mapenzi itajileta. Watoto huwa kwetu."

Pia alifichua kuwa alipogura ndoa yake, Vincent alioa mwanadada mwingine ambaye alitoroka kwa sababu ya mwanamke anayeishi na mumewe.

"Shughulika na wale uko nao. Miaka kumi nikivumilia sio mchezo. Nitashughulikia tu watoto wangu," alisema.

Huku akitetea mke wake mwingine, Vincent alisema, "Si mzee. Yeye ako na mwili nzito ndio maana anasema hivyo."

Dorice alisema, "Yeye mwenyewe ako na 31, mama ako na 38. Ndio nilikuwa nampenda lakini. Kama atakubali kusaidia watoto ni sawa, kama hatakubali ni sawa."