Patanisho: "Alipata kwa barabara?" Jamaa aruka mimba ya mwanadada aliyekutana naye tiktok

Stano alipinga kwamba mpenziwe ana ujauzito wake huku akidai vipimo vya awali vilikuwa vimeonyesha sio mjamzito.

Muhtasari

•Lucy alisema kuwa mahusiano yake ya chini ya mwaka mmoja yalisambaratika mwezi uliopita kufuatia tabia ya mpenziwe kutoa siri zao nje ya ndoa.

•Stano hata hivyo alionekana kutokuwa tayari kurudiana na mpenziwe na akaibua malalamishi mazito dhidi yake.

Image: RADIO JAMBO

Mwanadada ambaye alijitambulisha kama Lucy Waceke ,20, kutoka Murang'a alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mpenzi wake Mukuwe Ronald almaarufu Stano ,24,  ambaye alikosana naye takriban mwezi mmoja uliopita.

Lucy alisema kuwa mahusiano yake ya chini ya mwaka mmoja yalisambaratika mwezi uliopita kufuatia tabia ya mpenziwe kutoa siri zao nje ya ndoa.

Alidai kuwa mumewe alimtema baada ya kumshawishi aende nyumbani.

"Tulipatana tiktok tukakuwa wapenzi. Mapenzi ikakuwa ikafika mahali nikaacha kazi akanioa. Siku za kwanza alikuywa mzuri, baadaye akaanza madharau. Alisema anataka kuenda nyumbani kwao. Akaniambia nirudi kwetu kwanza atanitumia nauli ili nirudi. Hajawahi kunitafuta tangu nikuje nyumbani," Lucy alisimulia.

Aliongeza, "Kuna wakati nilikuwa mgongwa. Jioni nilirudi kama nimechelewa. Nilipata akiongea na rafiki yake akamwambia mambo yetu mpaka ya ndani. Hata hivyo, mimi nishamsamehe. Nikiskia vile atasema naweza kurudi."

Stano alipopigiwa simu, Lucy alichukua fursa hiyo kumuomba msamaha na kumweleza kwamba angependa kurudi.

Stano hata hivyo alionekana kutokuwa tayari kurudiana na mpenziwe na akaibua malalamishi mazito dhidi yake.

"Mimi nilikuwa naenda matanga nikakwambia uende kwenu ndo usiteseke. Alikuwa anasikiliza watu sana. Rafiki yake alianza kumwambia nimeenda nyumbani na nimeleta mwanamke ambaye ana mtoto. Na mimi nilikuwa nimeenda matanga," Stano alisema.

Aidha, alisikika kupinga madai ya mpenziwe kwamba ana ujauzito wake huku akidai kwamba vipimo vya awali vilikuwa vimeonyesha sio mjamzito.

"Alikuwa ashapima na akanionyesha hana mimba. Kwani alipata kwa barabara? Ulipataje mimba na ukiwa hapa ulipima na ukapata hauna mimba?.. Kama ako na mimba, azae mtoto nitalea. Lakini mimi sitakaa na mtu anasikiliza maneno ya nje," alisema Stano.

Huku akijitetea, Lucy alisema, "Pia mimi nimejulia nyumbani kwamba nina mimba."

Walipoambiwa waambiane maneno ya mwisho, Stano alisema ,"Akipata mtu mwingine, ikae kwa bwanake. Sio kusikiliza marafiki zake."

Lucy naye alisema, "Pia yeye akipata bibi mwingine aache kutoa maneno nje ya ndoa. Na ajue nilikuwa nampenda."

Je, una ushauri au maoni yepi kuhusu Patanisho ya leo?