•Cosmas alisema uhusiano wao uliharibika baada ya yeye kushindwa kutimiza ahadi ambayo alikuwa amempa kakake.
•"Stephen, mimi nimeshukuru sana kwa vile umenisamehe. Sina maneno ya kukwambia kwa vile umekuwa zaidi ya ndugu," Cosmas alijibu
Cosmas Maundu ,31, kutoka Thika alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na kakake mkubwa Stephen Makau ,36, ambaye alikosana naye takriban miezi miwili iliyopita.
Cosmas alisema uhusiano wao uliharibika baada ya yeye kushindwa kutimiza ahadi ambayo alikuwa amempa kakake.
"Huyo kakangu alinikasirikia. Kuna ahadi nilikuwa nimempea, nikakosa kupata. Nilijaribu kumuelezea, nikaona ni kama tutakosana zaidi. Sasa haniongeleshi hata kidogo," Cosmas alisema.
Aliongeza, "Yeye ni kaka yangu ambaye amenisaidia kwa miaka mingi. Wakati tunasaidiana, ni kusaidiana tu si kukopeshana. Alikuwa anatarajia sana hiyo pesa. Ni kama alikuwa anaona namhepa."
Stephen alipopigiwa simu, Cosmas alichukua fursa hiyo kumuomba msamaha na kumuomba warejeshe uhusiano wao.
"Kulingana na vile tulikuwa tumesema kabla ya kunyamaziana. Nilishindwa kutimiza yenye tulikuwa tumeahidiana. Nimeona nipitie mahali ndio tuwasiliane. Nilikuwa naomba msamaha. Nikikumbuka vile ulinisaidia, ni baraka kubwa na sitaki kuharibu. Naomba unisamehe ndio tuweze kurejesha uhusiano wetu kama ndugu," Cosmas alimwambia nduguye.
Stephen alimwambia, "Mimi sina ubaya na wewe. Nilijaribu kukupigia, sikukupata, niliona labda umeona kama sina maana kama ndugu. Nikaona niendelee na maisha yangu. Lakini vile umeomba msamaha, mimi nimekusamehe kama ndugu yangu. Tunaweza kuzika uhasama wote na kurejesha uhusiano kama ndugu."
"Stephen, mimi nimeshukuru sana kwa vile umenisamehe. Sina maneno ya kukwambia kwa vile umekuwa zaidi ya ndugu," Cosmas alijibu.
Katika ujumbe wake wa mwisho, Stephen alimwambia nduguye, "Ubarikiwe sana, na unitafute."
Je, maoni yako kuhusu Patanisho ya leo ni yepi?