Patanisho: Jamaa aoa mke mwingine kumwadhibu mkewe kwa kutishia kumuua kwa kisu

Wanjala aliomba kupewa mwaka mmoja unusu kabla ya kuamua iwapo Juliet atarudi.

Muhtasari

•Juliet alieleza kwamba ndoa yake ya miaka mitano ilisambaratika Oktoba mwaka jana baada ya kumfumania mumewe na mpango wa kando.

•Wanjala alifichua kuwa mkewe aliwahi kutishia kumuua baada ya kuzozana, jambo lililofanya amuadhibu kwa kutafuta mwingine.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Juliet ,24, kutoka Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Moses Wanjala ambaye alikosana naye mwaka jana.

Juliet alieleza kwamba ndoa yake ya miaka mitano ilisambaratika Oktoba mwaka jana baada ya kumfumania mumewe na mpango wa kando.

"Tulikuwa tumeoana, nilimpata na mpango wa kando, alikuwa kazi Naivasha na mimi nilikuwa nakaa nyumbani," alisimulia.

Mwanadada huyo alifichua kuwa Wanjala alikuwa anashika simu zake mchana tu ila ifikapo mida ya usiku hakuwa anapatikana.

"Ikifika kitu saa moja, saa mbili hivi simu ilikuwa inasema 'user busy'. Siku moja nilitoka nje kidogo nikaacha simu, kurudi nilipata nimetusiwa 'malaya wewe'. Nilimuuliza kwa nini amenitusi akasema alikuwa ameacha simu kwa moto hajui ni nani aliandika kwa kuwa alikuwa ameacha mlango wazi," alisema.

Juliet alifichua kuwa alimfumania mumewe na mwanamke mwingine wakati alipomtembelea kwake Naivasha.

"Mwezi wa kumi alinitumia pesa. Nilikuwa najua mahali anakaa. Nilimpata na mwandada mwingine kwa nyumba, tulizozana alikasirika akanichapa, nilienda kwa polisi alafu nkarudi kwangu nyumbani," alisema.

Alisema kwamba tangu wakati huo Wanjala hajakuwa akishika simu zake na hata hajakuwa akiwashughulikia watoto wao.

Wanjala alipopigiwa simu alidai Juliet alikuwa amemkosea vibaya kabla ya kufanya maamuzi ya kutafuta mwanamke mwingine.

Alifichua kuwa mkewe aliwahi kutishia kumuua baada ya kuzozana, jambo lililofanya amuadhibu kwa kutafuta mwingine.

"Maneno ulinifanyia  moyo wangu bado haujatulia. Wewe mwenyewe unajua ulichonifanyia," alimwambia Juliet.

Wanjala alisimulia, "Iko wakati tulizozana kidogo. Alitaka kunidunga na kisu. Yeye ndiye alisababisha nikawa na mpango na kando. Kabla atake kinitoa roho, niliamua kumtafutia mwanamke mwingine."

Alifichua kwamba Juliet alitaka kumuua baada ya mzozo wa kinyumbani kutimbuka kati yao.

"Tulizozana mambo ya nyumba kidogo. Alichukua glasi akataka kunirushia lakini nikahepa. Niliona adhabu ni mwanamke mwingine... Roho yangu haijatulia. Mimi sikumfukuza, yeye ndiye aliondoka," alisema.

Kufuatia hayo, Wanjala aliomba kupewa mwaka mmoja unusu kabla ya kuamua kama mzazi huyo mwenzake atarudi.

"Nataka arudi kwa sababu ako na familia yangu. Mambo ya familia yangu nitashughulikia, lakini kurudiana anipatie muda. Wacha nifikirie," alisema.

Katika utetezi wake, Juliet alikiri kwamba alitaka kumgonga mumewe kwa kosa ambalo alikuwa amemfanyia.

"Nilishika panga kwa sababu alikuwa ananipiga. Aliniitisha na nikampatia. Sikutaka kumuua," alisema.

Juliet alisema mzazi huyo alimfahamisha kwamba amesitisha mahusiano na mwanamke huyo mwingine ila anaona kama kwamba anamtania tu.

"Makosa ambayo Juliet alifanya bado yananiuma. Ndio maana nimepatia yeye mwaka moja na nusu. Mke huyo mwingine alienda nyumbani kidogo. Bado tuko na mahusiano na yeye," Wanjala alisema.

Juliet alimsihi Wanjala warudiane ili waweze kulea watoto wao pamoja. Pia alibainisha kuwa yuko tayari kuwa na mke mwenza.

Wanjala kwa upande wake alimtaka mzazi huyo mwenzake arekebishe tabia kabla ya kurudi huku akimhakikishia kwamba bado anampenda.