Mwanadada adondokwa na machozi hewani akisimulia jinsi anavyokosa mapenzi katika ndoa yake

Muhtasari

•Esina alisema mumewe hajawahi kurejea baada ya kuondoka  nyumbani takriban mwaka mmoja uliopita.

•Esina aliwezwa na hisia na hata kushindwa kuzuia machozi akisimulia masaibu yaliyokumbwa ndoa yake.

Ghost Mulee studioni
Ghost Mulee studioni
Image: RADIO JAMBO

Esina Nyanganyi alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Charles Njoro ambaye hajaonekana nyumbani kwa muda mrefu.

Esina alisema mumewe hajawahi kurejea baada ya kuondoka  nyumbani takriban mwaka mmoja uliopita.

Licha ya kuwa mumewe amekuwa akituma pesa za matumizi ya nyumbani, Esina alisema ana wasiwasi mkubwa kuhusu ndoa yao kwa kuwa ameyakosa sana mapenzi.

"Huwa anatuma pesa vizuri. Hata jana alituma pesa ya mtoto ya shule. Lakini tangu Julai hata siku moja hakuji. Nikimuuliza huwa anakata simu. Huwa anasema atakuja Ijumaa wiki ijayo lakini ikifika anasema ameshindwa kuja. Huwa anafanya kazi ya juakali," Esina alieleza.

Esina aliweka wazi kwamba licha ya kuwa hajaweza kumuona mumewe kwa kipindi cha miezi mingi bado amesalia kuwa mwaminifu katika ndoa yao na kamwe hajawahi kutoka nje.

Charles alipopigiwa simu alizungumza kwa muda mfupi ila akakata mara moja punde baada ya kuulizwa sababu zake kutofika nyumbani.

Kutokana na hayo Esina alitangaza kuwa hataweza  kuendelea kuvumilia tena  pale nyumbani bila mumewe.

"Nimefika mwisho. Nimeng'ang'ana kila mahali. Nimeteseka ya kutosha. Nakazana hapa pekee yangu lakini hakuji. Hata mwezi Desemba mtoto wetu wa miaka mitatu alikunywa sumu ya ngombe akalazwa hospitali lakini hakuja," Alisema Esina.

Esina alisema hajaweza kuenda kumtafuta mumewe kwa kuwa anahofia huenda Charles akazima simu punde akijua anamtafuta.

Esina aliwezwa na hisia na hata kushindwa kuzuia machozi akisimulia masaibu yaliyokumbwa ndoa yake.

Baba mkwe wa Esina alithibitisha malalamishi ya Esina huku akisema mwanawe amekuwa akiahidi kurudi  nyumbani bila kutimiza ahadi yake. Hata hivyo alimwomba mkwe wake aendelee kuvumilia.

"Ata mimi nimeshindwa kwa sababu hajawahi kuja nyumbani. Saa zingine huwa anaongea na mimi. Huwa anasema atakuja lakini hakuji," Baba Charles alisema.